×

Utafiti Wabaini Kukithiri Kwa Rushwa ya Ngono Kwenye Vyombo vya Habari

 

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Februari 17, 2023  kimeendesha mjadala na wahariri wa vyombo vya habari kujadili rushwa ya ngono katika tasnia ya habari ili kubaini changamoto na kuona namna bora ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo utafiti umeonyesha limekithiri ndani ya vyumba vya habari.

 

Utafiti uliofanyika kuhusu rushwa ya ngono katika vyombo vya habari na TAMWA tangu mwaka 2020, umebaini kuwa zipo sababu kadhaa ambazo zinachangia tatizo la rushwa ya ngono.

 

Sababu ya kwanza imetajwa kuwa ni kwa baadhi ya waandishi wa habari wa kike, kutengeneza mazingira ya kuombwa penzi na wahariri au wazalishaji wa vipindi (producers) ili wapate upendeleo na urahisi kwenye shughuli zao wawapo kazini.

 

 

Sababu nyingine imetajwa kuwa ni kukosa maadili kwa baadhi ya wahariri na wazalishaji wa vipindi, ambapo hutumia vyeo na nafasi zao kuwalazimisha waandishi wa habari wa kike kuingia nao katika uhusiano wa kimapenzi.

 

Sababu ya tatu, imetajwa kuwa ni kwa baadhi ya waandishi wa habari wa kike wasio na uwezo wa kutimiza majukumu yao ya kikazi, kutengeneza mazingira ya kusaidiwa kazi zao ili kulinda ajira zao ambapo mwisho hutoa rushwa ya ngono kama shukrani.

 

 

Utafiti huo umeyataja makundi matatu yanayoongoza kwa kuomba rushwa ya ngono kwa waandishi wa habari wanawake ambapo kundi linaloongoza ni wazalishaji wa vipindi (producers) wakifuatiwa na wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari.

 

Tatizo la rushwa ya ngono kwa waandishi wa habari, limeelezwa kuwa lipo kwa muda mrefu lakini haliripotiwi kwa sababu mbalimbali na hivyo kufanya hatua za kulidhibiti zisichukuliwe.

 

Miongoni mwa sababu zinazofanya tatizo hilo lisiripotiwe, ni kwa waathirika wa kuombwa rushwa ya ngono, kuogopa kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili huo kwa kuhofia kufukuzwa kazi au kuharibiwa maisha na waliowafanyia vitendo hivyo.

 

Sababu nyingine, ni kukosekana kwa sera madhubuti juu ya namna ya kushughulikia matatizo haya yanapojitokeza ndani ya vyumba vya habari.

 

Ili kukabiliana na tatizo hili, utafiti wa TAMWA umependekeza kuwepo na sera madhubuti za kusimamia maadili ya kazi ndani ya vyiombo vya habari lakini pia waandishi wa habari, wapewe elimu ya kutosha kuanzia wakiwa vyuoni juu ya namna ya kukabiliana na tatizo hili ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo.

Leave a Comment