
Kufuatia mjadala wa Kitaifa wa nishati safi ya kupikia na azma ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama kuni kichwani, Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TABWA), imeandaa kongamano la Nishati Safi ya Kupikia litakalofanyika tarehe 22-24 mwaka huu katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki- Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TABWA, Noreen Mawalla wakati akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni.Lengo la kongamano hilo ni kutoa elimu, kupanga mikakati ya utekelezaji na kujenga mtandao wa Biashara.
Noreen amesema kwenye kongamano hiloo walengwa wakuu ni wanawake, vijana, wauza mkaa, watengenezaji na wauzaji wa majiko ya nishati safi, wamiliki wa migahawa, shule, hoteli, vyuo, wataalam wa afya na mazingira na wadau wengine.

Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa wadau wote hao kuhudhuria kongamano hilo ili wapate elimu na kujenga mtandao wa kibiashara kupitia nishati safi ya kupikia. Katika kongamano hilo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nishati, Januari Makamba amekuwa akisisitiza kutumia nishati safi.