
SPIKA wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson asubuhi ya leo Juni 27,2023 ameahirisha shughuli za Bunge kwa muda baada ya kengele ya tahadhari kulia ndani ya ukumbi wa Bunge.
Mara baada ya kuibuka kwa hali ya sintofahamu katika ukumbi wa Bunge na kupelekea kuahirishwa kwa shughuli za Bunge kwa muda, Dkt. Tulia Ackson ametoa ufafanuzi kuhusiana na hali hiyo iliyojitokeza Bungeni hapo.
Katika ufafanuzi wake, Spika wa Bunge amesema kwamba hali hiyo imesababishwa na vifaa maalumu ambavyo vinahusika na kuhisi moshi kwenye jengo hilo kufanikiwa kunasa vumbi na kisha kulitafsiri kama moshi kwasababu ya ukarabati unaoendelea katika vyumba vilivyopo chini ya ukumbi wa Bunge kutokana na kwamba vyumba hivyo hutumika kwa kazi nyingine.
Aidha, Dkt. Tulia ametoa maelekezo kwa wabunge pamoja na wageni wote wanaotembelea Bunge kwamba endapo kunatokea dharura wakati mwingine, kila mmoja anatakiwa kutoka Bungeni hapo kupitia mlango uliopo karibu naye na kisha aelekee lango C mahali ambapo watakusanyika ili kuweza kupewa taarifa juu ya kile kilichotokea.