×

Majaliwa: Mfuko Wa Watu Wenye Ulemavu Haujaunganishwa Na Mifuko Mingine

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mfuko wa Taifa kwa Watu wenye Ulemavu haujaunganishwa na mifuko mingine ya makundi maalum kama ambavyo inadaiwa.

“Katika risala yenu mmeomba Mfuko wa Taifa kwa Watu wenye Ulemavu usiunganishwe na mifuko mingine ili uweze kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa kwenye Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010.

Nitumie fursa hii kuwafahamisha kuwa mfuko huo haujaunganishwa na mifuko mingine na kama mlivyosikia, mfuko huo umetengewa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali kwa watu wenye ulemavu,” amesema.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Agosti 5, 2023 wakati akifungua kongamano la siku moja la watu wenye ulemavu Dar es Salaam lililofanyika kwenye ukumbi wa JNICC, jijini humo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua Taasisi Kusaidia Watu Wenye Ulemavu (KEDEF) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimatyaifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Agosti 5, 2023. Wa tano kushoto ni Mwenyekiti wa Taasisi Kusaidia Watu Wenye Ulemavu (KEDEF), Khadija Taya maarufu kwa jina la Keysha, wa tatu kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Watu Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Rasheed Maftah.

Alikuwa akijibu hoja kuu ya kwenye risala ilisomwa na Mwenyekiti wa SHIVYAWATA, Ernest Kimaya ambaye alitaka wapate majibu ya Serikali kuhusu hatua iliyofikiwa ya uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Watu wenye Ulemavu kwani wanaona ukiunganishwa na mifuko mingine, utasababisha masuala yao yafunikwe na kundi lao halitanufaika ipasavyo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuainisha changamoto zitakazowakabili kwenye matumizi ya fedha hizo endapo hawatajipanga kwa vile wana makundi mengi ambayo inabidi yaainishwe ili kila kundi liweze kunufaika na mfuko huo.

“Watu wenye ulemavu mna makundi mengi mno kama walivyo wasanii. Kuna wasanii wa muziki wa bongo fleva, orchestra, muziki laini, wa kufoka foka, bongo movie, wachoraji na wachongaji. Na hapa nimeona huo mchanganyiko. Mwenyekiti inabidi mkae na kuainisha haya makundi ili muweze kunufaika,” amesema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mkwamo wanaoupata watu wenye ulemavu katika maombi ya kazi kupitia utaratibu wa kidijitali wa Sekretarieti ya Ajira, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua uwepo ya changamoto hiyo na tayari imeweka utaratibu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

WAZIRI MKUU MAJALIWA – “TUTUMIE ZANA za TEKNOLOJIA KUBORESHA SEKTA ya KILIMO, UVUVI na UFUGAJI”…

Leave a Comment