
Shule za sekondari nchini zimeaswa kuiga mfano wa shule ya Sekondari ya St Mary Goreti katika utendaji wa mambo mbalimbali ikiwemo elimu na michezo.
Hayo yalisemwa na Kamishna wa Skauti Wilaya ya Moshi, Bi Emerensiana Mbena ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mbio za hisani za km 10 na km 5 zilizoandaliwa na shule hiyo hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuadhimisha Jubilee ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.
“Kwa kweli St. Mary Goreti mmedhihirisha kuwa nyinyi sio wazuri kwenye elimu tu bali hata kwenye michezo. Mbio za leo zimefanyika kwa weledi mkubwa na tumeona jinsi gani kuna vipaji hapa,” alisema Bi Mbena.

Natoa wito kwa shule zingine ziige mfano huu wa St Mary Goreti kwa kubuni njia mbalimbali za kujiletea maendeleo. “Mwaka kesho St Mary Goreti wanaadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa na wamebuni njia tofautitofauti za kuhamasisha uchangiaji katika harambee ya kufanikisha jubilee hii mojawapo ikiwa ni mbio na matembezi ya km 10 na Km 5,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro, Abraham Mikumi, alisema St Mary Goreti wameonesha mfano mzuri wa kuigwa na shule zingine za Mkoa wa Kilimanjaro ili kukuza vipaji hasa katika mchezo wa riadha.
“Tunawashukuru kwa kutushirikisha maana kama chama cha riadha tunaweza kupata vipaji ambavyo vitakuzwa na kulitumikia taifa katika mashindano mbalimbali. Hii ni shughuli kwa ajili ya kuchangisha fedha lakini pia kuna kipengele cha mashindano,” alisema.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo pia aliwapongeza wadhamini wa mbio hizo za St Mary Goreti wakiwemo Kilimanjaro Water na kampuni ya simu ya TIgo kwa kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ufanisi.
“Tumeshuhudia maji ya kutosha katika vituo vya maji na yote haya yamewezeshwa na wenzetu wa Kilimanjaro Water kwani bila maji washiriki wangepata shida sana lakini Tigo nao wamerahisisha namna ya wadau kuchangia katika harambee hii kwa kutoa LIPA NAMBA 7945925,” alisema.
Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St Mary Goreti Sr. Cleopha Saritha alisema walichagua kufanya mbio kama namna ya kuimarisha afya na kuhamasisha wananchi kuhusu harambee hiyo inayolenga kukufanya Milioni 600 kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya shule hiyo kabla ya sherehe za jubilee ya miaka 25 hapo mwakani.
Mbio hizo, zilizofanyika katika Uwanja wa Ushirika Moshi (MoCU) na kuratibiwa na Kampuni ya Executive Solutions Ltd, ziliwakusanya zaidi ya washiriki zaidi ya 900 wakiwemo wanafunzi, wazazi, walimu na wananchi wa kawaida.