
Nyumba ya Meya wa mji wa Derna uliopo Libya imechomwa moto wakati mamia ya waandamanaji wakitaka majibu kuhusiana na janga la mafuriko makubwa lililoikumba nchi hiyo wiki iliyopita.
Katika mafuriko hayo yaliyosababishwa na kimbunga Daniel mji wa Derna ndio ulioathirika vibaya kuliko sehemu zingine zote.
Watu hao walikusanyika jana usiku katika msikiti wa Sahaba ambao ni alama ya kihistoria ya mji huo, wengi wao wakiimba na kuwataka maafisa wa serikali ya Libya mashariki kufukuzwa kazi.
Hadi sasa halmashauri yote ya jiji la Derna imekwisha fukuzwa kazi.
Mitandao ya intaneti na simu imekatwa na waandishi wa habari wameamriwa kuondoka, jambo ambalo ni ukandamizaji wa vyombo vya habari.
Zaidi ya watu 10,000 wametajwa kupotea katika mji wa Derna pekee baada ya mabwawa mawili yaliyochakaa kupasuka na kuujaza mji huo kwa maji.
Akizungumza kutokea hospitali alikolazwa, mmoja wa majeruhi amesema ”mimi na watu wengine tuliionya sana halmashauri, tukisihi mabwawa yakarabatiwe baada ya kuona yakivuja miaka miwili iliyopita”.
Idadi kamili ya vifo bado haijajulikana, hata hivyo watu zaidi ya 4,000 wamethibitishwa kupoteza maisha.
Hivi sasa mashirika kadhaa ya uokoaji na utoaji wa misaada ikiwemo Umoja wa Mataifa yamezuiliwa kuingia Derna.