
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amewakaribisha wawekezaji kutoka Norway kuja kuwekeza nchini kwenye sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi na kukuza uchumi wa nchi ikiwemo nishati mbadala, kilimo, gesi na mafuta, mifuko ya uwekezaji na usafirishaji.
Mhe. Rais Samia ametoa wito huo alipohutubia Wajumbe walioshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway liliofanyika jijini Oslo, tarehe 13 Februari 2024
Mhe. Dkt. Samia ambaye aliongozana na Mwana Mfalme wa Norway Haakon kwenye Kongamano hilo amesema Tanzania inahitaji wawekezaji wenye nia thabiti kuja kuwekeza mitaji yao nchini kwenye sekta ambazo kwa kiasi kikubwa zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kama vile chakula, umeme, mafuta na usafirishaji.
Amesema Tanzania ni sehemu salama kwa wawekezaji kutoka Norway kuwekeza mitaji yao kwakuwa Serikali imeboresha sheria mbalimbali za uwekezaji na kwamba kijografia Tanzania inafikika kwa urahisi na inapakana na nchi nane ambazo ni soko kubwa kwa wawekezaji na pia Tanzania ni nchi ya amani inayoamini katika usawa na utawala wa sheria.

Akizungumzia kilimo, Mhe. Rais Samia amewaeleza wawekezaji hao kwamba bado sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania haijatumika ipasavyo kwenye sekta ya kilimo ambapo zipo Hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo na kati ya hizo Hekta milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji
Ameongeza kuwa, Tanzania ni nchi ya 10 duniani kwa uzalishaji wa zao la Alizeti na ni nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa zao hilo ambalo bidhaa zake ikiwemo mafuta zinahitajika kwa wingi nchini na nchi jirani.
Kuhusu nishati mbadala, Mhe. Rais Samia amewahamasisha wawekezaji hao kuchangamkia fursa za umeme wa jua na upepo kwani bado Tanzania inahitaji kuwa na uhakika wa upatikaji wa nishati mbalimbali ikiwemo umeme wa uhakika.
Awali akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kuhamasisha wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi na namna ambavyo ameendelea kutambua mchango wa sekta binafsi kwenye uchumi na maendeleo ya nchi.