
Jopo la wajumbe wa mahakama moja mjini New York, Alhamisi limempata na hatia rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kwa mashtaka 34 ya kugushi hati zake za biashara.
Washington —
Jopo la mahakama la wajumbe 12 lilitathmini na kutafakari kwa siku mbili ushahidi wote liliopokea na kutoa uamuzi dhidi ya Trump mwenye umri wa miaka 77 , katika kesi ya kwanza kabisa ya uhalifu dhidi ya rais wa zamani wa Marekani.
Wakili wa Trump, Todd Blance aliomba uamuzi huo wa kupatikana na hatia ubatilishwe, lakini hakimu wa Mahakama Kuu ya New York Joan Merchan mara moja alipinga hoja hiyo.
Trump alipatikana na hatia kutokana na mashtaka kwamba alimlipa Stormy Daniels, mwanamke muigizaji wa filamu za ngono karibu dola 130, 000 ili kumnyamazisha, inayofahamika kama “hush money” kabla ya uchaguzi mkuu wa 2016.
Hukumu ya Trump imepangwa kutolewa Julai 11, kati kati ya kampeni yake ya kujaribu kurudi kwenye White House, siku chache tu kabla ya kuanza kwa Kongamano la Kitaifa la chama cha Republican hapo Julai 15.
Trump bado anatarajiwa kugombania kiti cha rais wakati wa uchaguzi wa mwezio Novemba dhidi ya Rais Joe Biden aliyemshinda wakati wa uchaguzi wa 2020.