
BARAZA la Ushindani la Taifa ( Fair Competition Commission) leo tarehe 3 Juni 2024 limehairisha usikilizaji wa kesi ya mgogoro wa kituo cha mafuta kilichojengwa katikati ya makazi mtaa wa Senga Mikocheni jijini Dar es Salaam hadi tarehe 18 Juni kesi itakapotajwa tena. Walalamikaji ni Profesa Anna Tibaijuka na wenzake 9. Walalamikiwa ni Kampuni ya mafuta ya Barrel Oetroleum na EWURA ambayo imeshitakiwa kwa kukataa kusikiliza shauri la mgogoro huo ikidai mgongano wa maslahi. Walalamikaji wanaitaka EWURA kuwajibika kwa mujibu wa sheria kama mamlaka pekee ya kuratibu shughuli zote za mafuta ikiwemo kutoa leseni.
Aidha Baraza la Ushindani limewakaribisha wadau wengine wa swala hilo kujitokeza kutoa maoni yao juu ya usahihi au vinginevyo kwa EWURA kukataa kutekeleza wajibu wake katika mgogoro huo ambapo vituo vya mafuta vilivyopo katika makazi ya watu unahitaji kusitishwa. Wadau wamepewa siku 7 hadi tarehe 7 Juni kuwa wamewasilisha maombi ya kuingilia shauri na kusajili maoni yao.
–
Desemba 14, 2023 Profesa Anna Tibaijuka na wengine tisa waliwasilisha malalamiko kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati (EWURA) dhidi ya kampuni hiyo wakilalamikia madai ya ujenzi wa kituo cha mafuta katika kiwanja Na. 411 barabara ya Senga mtaa wa Ali Hassan Mwinyi Mikocheni, Dar es Salaam kuwa kilijengwa katika maeneo ya makazi kinyume cha sheria.
–
Katika taarifa yao Baraza la Ushindani limesema kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa leo Juni 3, 2024 lakini imehairishwa mpaka Juni 18 mwaka huu.
–
Desemba 23, 2023, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa alisimamisha matumizi ya kituo cha mafuta cha Barrel Petrol Energy cha Mikocheni na kutamka bayana mchakato wa kubadlisha matumizi y atdhi ulikuwa na kasoro. Waziri Slaa alipiga marufuku ujenzi holela wa vituo vya mafuta nchi nzima vinavyojengwa kwenye makazi ya watu hatua inayohatarisha usalama wa watu na mali zao.
–
Akiwa eneo lililojengwa kituo hicho cha mafuta, Waziri Silaa aliagiza wakuu wote wa Idara ya Ardhi na Mipango miji nchi nzima wafanye uhakiki wa vituo vya mafuta kwa maana ya viwanja, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, mchakato uliotumika, ukubwa wa viwanja, ukaribu wa kituo kimoja na vituo vingine na ukaribu wa maeneo mengine ya kutolea huduma za jamii, hali ya uendeshaji wa vituo hivy na taarifa hizo zilipaswa kufika ofisini kwake Januari 31, 2024.
|
|