×

Teknolojia ya Uhimilishaji Kutoka Marekani na Brazil Kuleta Mapinduzi Sekta ya Mifugo

 

 

Wafugaji wazawa sasa wanaweza kuongeza uzalishaji wao wa maziwa na nyama kufuatia kufikiwa na teknalojia mpya na ya kisasa ya uhimilishaji ambayo imefanyiwa utafiti wa kina kutoka nchini Marekani na Brazil.

Teknolojia hiyo mpya inayohusisha kuchanganya mbegu za ng’ombe wa asili na mbegu za kutoka Marekani na Brazil ambapo hupelekea kupatikana kwa ng’ombe chotara imeletwa hapa nchini na kampuni ya URUS inayojihusisha na usambazaji wa mbegu bora za ng’ombe wa nyama na maziwa duniani.

Akiongea katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, meneja mkazi wa URUS Tanzania Edson Mfuru alisema ng’ombe wanaozalishwa kupitia uhimilishaji wanaoufanya wana uwezo mkubwa wa kuzalisha maziwa na nyama ukilinganisha na mbegu za asili.

Pamoja na kwamba Tanzania ni nchi ya pili kwa wingi wa mifugo barani Afrika baada ya Ethiopia, mchango wa sekta hii kwa pato la taifa bado ni mdogo. Sababu zinazotajwa kupelekea mchango mdogo ni pamoja na matumizi ya mbegu za asili ambazo zinatoa uzalishaji mdogo.

Meneja mkazi huyo anasema wakati mbegu za asili zikitoa maziwa kati ya lita 1-5 kwa siku, ng’ombe chotara ambao huzalishwa kwa kutumia mbegu wanazotoa Brazil na Marekani huzalisha kati ya lita 15-25 kwa siku hivyo kumhakikishia faida mfugaji.

Kwa upande wa nyama anasema mbegu za asili zinauwezo wa kutoa kiwango cha juu kabisa cha nyama kilo 200 wakati ng’ombe chotara wanaotokana na mbegu zao huweza kutoa hadi kilo 1,000

“Uhimilishaji ambao hupelekea kupatikana kwa ng’ombe chotara kama Girolando, hufanyika ili kubadilisha chakula kuwa misuli kwa ufanisi zaidi. Chakula kidogo huitajika kwa ajili ya kuzalisha kiasi kikubwa zaidi cha maziwa au nyama. Matumizi ya chakula kidogo kulisha ng’ombe husaidia kupunguza gharama za ulishaji ambazo huwa kubwa katika ufugaji.”

Mfuru alisema kwa sasa URUS Tanzania inafanya kazi na wafugaji katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Iringa, Njombe, Mbeya na Kagera, ikiwapa elimu juu ya mbegu bora na pia kuwapatia mbegu zilizoboreshwa katika maeneo yao.

“Ingawa kwa sasa tunapatikana katika maeneo niliyoyataja, lengo letu ni kuwafikia wafugaji popote walipo hapa Tanzania. Madhumuni yetu ni kuhakikisha kila mfugaji anafikiwa popote pale alipo na kupatiwa huduma zitakazomsadia kuboresha ufugaji wake. Tunaendelea kujitanua na kuboresha huduma zetu ili kukidhi mahitaji ya wafugaji wote,” aliongeza.

Leave a Comment