×

Prof. Kabudi Aagiza Waliong’oa Viti Kwa Mkapa Wakamatwe

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Profesa Kabudi

Kufuatia fujo zilizotokea na kupelekea mashabiki kung’oa na kuharibu viti vya kukalia watazamaji katika uwanja wa Benjamin Mkapa wakati wa mchezo wa hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji, Simba Sc dhidi ya Club Sportif Sfaxien ya Tunisia uliofanyika jana tarehe 15 Desemba, 2024, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi ameagiza waliohusika katika uharibifu huo wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria.

Taarifa ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeeleza kwamba Mhe. Prof. Kabudi amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuchukua hatua mara moja kwa kuwaandikia Simba Sc na kuwanakili Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) ili gharama za uharibifu uliosababishwa wakati mechi hiyo zilipwe.

Mhe. Waziri Kabudi amewataka mashabiki wanaoingia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuacha vitendo vya uharibifu wa uwanja kwa kuwa wanasababisha hasara kwa Serikali na kuharibu ubora wa uwanja.

“Vitendo vilivyofanyika jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa havikubaliki na sio vya kimichezo, nakuelekeza Katibu Mkuu kuchukua hatua mara moja. Pamoja na kuwaandikia Simba Sc na TFF, wapeni ushirikiano Polisi ili watu wote waliokuwa wanang’oa viti na kuvitupa wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria, lazima tabia hii ikomeshwe” amesema Prof. Kabudi.

KAMANDA MULIRO ATOA TAMKO VURUGU MECHI ya SIMBA – ”VITI 256 VIMENG’OLEWA – SHABIKI 1 MAJERUHI”…

Leave a Comment