
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara na mtia nia nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Tundu Antiphas Lissu leo ametoa salam za mwaka mpya 2025 kupitia vyombo vya habari.
Katika salamu hizo, Lissu amezungumza mengi kuhusiana na hali ya kisiasa ndani ya chama chake na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 Lissu alisema:
“Kwa kifupi, kuanzia sasa, kama tutashiriki tena kwenye chaguzi zijazo, ukiwemo Uchaguzi Mkuu wa 2025, bila kuwa na Katiba Mpya ya kidemokrasia, na bila ya kuwa na mfumo mpya wa kidemokrasia wa uchaguzi wenye Tume Huru ya Uchaguzi na Sheria Mpya za Uchaguzi, tutashiriki huku tukijua fika kwamba wapiga kura feki wataandikishwa, wagombea wetu wataenguliwa, tutafanyiwa kila aina ya vurugu kwenye kampeni na siku za uchaguzi, kura halali zitaibiwa na kura feki zitaingizwa na wagombea walioshindwa watatangazwa washindi wa chaguzi hizo.”
Akaongeza: “Ukweli huu mchungu unatutaka tubadilishe mbinu za mapambano ya kidemokrasia. Tumesubiri CCM na serikali zake wabadilishe msimamo wao kuhusu Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi kwa miaka mingi. Tumewabembeleza kwa muda mrefu wakubali nchi yetu iondokane na katiba ya sasa ambayo, kwa misingi na maudhui yake, ni katiba ya chama kimoja na ya utawala wa kiimla.
“CCM na serikali zake imeshauriwa na wataalamu iliyowateua yenyewe, wengi wao wakiwa wanaCCM, kwamba nchi yetu inastahili kuwa na Katiba Mpya ya kidemokrasia itakayokuwa na mfumo huru wa uchaguzi.”
Akizungumzia uchaguzi ndani ya Chadema Lissu amesema wajumbe wa uchaguzi walipiwe nyumba zakulala wageni na usafiri wa kwenda na kurudi makwao ili kuzuia rushwa ndani ya chama.
Ametoa rai kwa wagombea wenzake katka uchaguzi huo wa chama kupiga vita rushwa ili wananchi waweze kukiamini chama.
Akasema wana wajibu wa kuhakikisha uchaguzi wao unakuwa wa amani huru na haki, na amewaasa wajumbe kuhakikisha wanaepuka vishawishi vyovyote vya uvunjifu wa amani wakati wote wa uchaguzi.
Alipendekeza viongozi wa dini na wawakilishi wa mabalozi kualikwa ili kuupa nguvu na hadhi uchaguzi huo na chama chao. Anataka ukomo wa uongozi kwa nafasi zote zikiwemo za ubunge wa viti maalum, alisema kipindi kimoja tu kinatosha kumpa uzoefu na kumuwezesha kwenda kugombea kwenye jimbo.
Stori na Elvan Stambuli | GPL