×

Rais Biden: Muuaji Alichochewa na Magaidi Wa IS

Rais wa Marekani Joe Biden

Rais wa Marekani Joe Biden amesema mhusika wa shambulizi la mjini New Orleans lililoua watu 15 na wengine 35 kujeruhiwa  alichochewa na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu- IS.

Akinukuu taarifa za Shirika la Upelelezi la Marekani FBI, Biden amesema saa chache kabla ya shambulio mhusika huyo alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii, zinazoashiria kwamba alihamasishwa na IS, akielezea shauku ya kuua.

FBI imemtambua mshambuliaji huyo kuwa ni Shamsud-Din Jabbar, raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 42 kutoka Texas. Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema Jabbar aliwahi kuhudumu katika jeshi kama mtaalamu wa rasilimali watu na mtaalamu wa Tehama kutoka mwaka 2007 hadi 2015 na kisha kikosi cha akiba hadi mwaka 2020.

Alitumwa Afghanistan kuanzia Februari 2009 hadi Januari 2010, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, akiongeza kuwa alikuwa na cheo cha Staff Sajenti mwishoni mwa utumishi wake.

Mkuu wa Polisi Anne Kirkpatrick amemtaja Jabbar kama “gaidi,” huku FBI ikisema “bendera ya IS ilikutwa ndani ya gari lililohusika kuvamia umati wa watu waliokuwa wanasherehekea Mwaka Mpya 2025.

Maafisa wa usalama bado wanatafuta wahusika wengine wa shambuliz hilo lakini hawakutoa maelezo ya kina huku afisa mwanadamizi wa FBI Alethea Duncan akionya kwamba mamlaka haiamini kuwa Jabbar alifanya uhalifu huo peke yake.

Leave a Comment