
Watu watano wamefariki dunia nchini Ujerumani huku afisa mmoja wa polisi akijeruhiwa kutokana na ajali zinazofungamana na matukio ya kurushwa kwa fataki za kusherehekea mwaka mpya 2025, hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya polisi nchini humo.
Msemaji wa polisi Florian Nath amesema maafisa 13 wa polisi wamejeruhiwa, akiwemo mmoja aliyepata majeraha mabaya kwenye vurugu hizo za sherehe za mwaka mpya.
Tarifa hiyo imesema watu 330 wamekamatwa katika mji mkuu Berlin usiku wa kuamkia leo huku taarifa ya polisi ikieleza kuwa, tofauti na miaka ya nyuma, mwaka huu mpya haukushuhudia matukio makubwa ya vurugu wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya.
Wajerumani husherehekea mwaka mpya kwa kurusha fataki, hali ambayo husababisha mijadala ya mara kwa mara juu ya kupiga marufuku fataki zinazoonekana kuwa hatari, hasa kutokana na idadi ya majeruhi kila mwaka, uchafuzi wa mazingira na kelele.