×

HAMAS Yasitisha Mchakato Wa Kuwaachia Mateka Wa Israel

Kikundi cha HAMAS kimetangaza kuwa, kinasitisha mchakato wa kuwaachia huru mateka wa Israel uliopangwa kutekelezwa Jumamosi ijayo hadi litakapotolewa tangazo jingine, kutokana na utawala wa Israeli kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa HAMAS Abu Obeida kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram imesema: “katika kipindi cha wiki tatu zilizopita, uongozi wa Hamas umefuatilia ukiukaji wa makubaliano unaofanywa na adui (Israel) na kushindwa kwake kuzingatia masharti ya makubaliano, ikiwa ni pamoja na kuchelewesha kurejea kwa watu waliohama makazi yao kaskazini mwa Ghaza, kuwalenga kwa makombora na risasi katika maeneo mbalimbali ya Ukanda huo, na kuzuia kuingia misaada ya kibinadamu ya aina zote kama ilivyo katika makubaliano”.

Abu Obeida ameongezea katika taarifa yake hiyo kwamba, kwa sababu hiyo, kuachiliwa wafungwa wa Israel, ambako kulipangwa kufanyika Jumamosi ijayo, kunaahirishwa hadi litakapotolewa tangazo jingine, ili kusubiri utawala wa Israeli utekeleze kikamilifu makubaliano na kufidia yale uliyoyakwamisha katika wiki zilizopita.

Kufuatia tangazo hilo, kwa niaba ya Waziri mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri wa Vita wa Israel Katz ameamuru jeshi la srael lijiweke tayari kwa kiwango cha juu kabisa cha tahadhari kwa ajili ya hali yoyote inayoweza kujitokeza huko Ghaza. Katz amedai kuwa tangazo la Hamas ni ukiukaji wa moja kwa moja wa makubaliano ya kusitisha mapigano.