
Viongozi wa Ulaya wametangaza kuunga mkono Ukraine katika mkutano wa kilele uliofanyika London, wakiahidi kuongeza matumizi katika usalama na kuunda muungano wa kulinda makubaliano yoyote ya amani nchini humo.
Mkutano huo uliowakutanisha washirika 18 ulifanyika siku mbili baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kumshambulia Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, mbele ya waandishi wa habari katika Ikulu ya White House.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alisema Uingereza, Ufaransa, na mataifa mengine yatashirikiana na Ukraine kuandaa mpango wa kusitisha mapigano, ambao utawasilishwa kwa Marekani. Aliongeza kuwa Ulaya ipo katika “njia panda ya kihistoria” na inapaswa kuchukua hatua bila kusubiri Marekani.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alisema yeye na Starmer wanapendekeza makubaliano ya muda ya amani ya mwezi mmoja, ambayo yatahusu usitishaji wa mapigano angani, baharini, na kwenye miundombinu ya nishati.
Zelensky alipokelewa vyema na viongozi wa dunia kwenye mkutano huo na akasema anaamini anaweza kurejesha uhusiano wake na Trump licha ya mvutano wao wa hivi karibuni. Alisisitiza kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Ukraine kwa kuwa mataifa mengi hayako tayari kumuacha Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ashinde.