The House of Social Media
gunners X

Msigwa: Serikali Imeumizwa na Upotoshaji wa Vyombo vya Habari vya Nje – Video

0
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Gerson Msigwa.

Dar es Salaam, Novemba 23, 2025 — Serikali imevitaka vyombo vya habari, hususan vile vya kimataifa, kuzingatia maadili, usawa na uwajibikaji katika kuripoti taarifa zinazohusu masuala nyeti nchini, ikisisitiza kuwa habari za upande mmoja zimeanza kuleta madhara makubwa kwa jamii na kuwagawa Watanzania.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Gerson Msigwa, akizungumza leo na waandishi wa habari katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam, amesema Serikali imesikitishwa na namna baadhi ya vyombo vya habari vya nje vinavyochapisha taarifa zisizo na mizani, nyingine zikiwa na upotoshaji unaolenga kuchochea chuki na migawanyiko ya kisiasa, kidini na kikanda.

“Tunapoendelea kusubiri tume hii ikamilishe kazi yake, kumejitokeza wimbi kubwa la vyombo vya habari hususani vya nje kuchapisha taarifa ambazo ni za upande mmoja na wakati mwingine kufanya upotoshaji wenye mrengo wa kuchochea chuki kwa Watanzania dhidi ya Serikali na kuwagombanisha wao kwa wao,” alisema Msigwa.

Amesema Serikali, pamoja na viongozi wake akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeumizwa na kusikitishwa na mwenendo huo ambao hauna manufaa kwa taifa, bali unaongeza maumivu katika yale maeneo ambayo Watanzania tayari wanapitia changamoto.

Msigwa amekemea vikali utetezi wa baadhi ya vyombo vya habari kwamba “Serikali haikupatikana” wakati wa kuandaa taarifa, akitoa mfano wa shirika la habari la kimataifa CNN ambalo lilichapisha taarifa zenye tuhuma bila kuipa Serikali nafasi ya kujibu.

“Sio haki na sio sawa kwa chombo cha habari kuchapisha taarifa za upande mmoja na kisha kutoa sababu kuwa maafisa wa Serikali walipotafutwa hawakupatikana kama ambavyo chombo cha CNN kilivyochapisha habari zilizojaa tuhuma pasipo kutoa nafasi ya Serikali kujibu,” alisema.

Aidha, Msigwa amevitaka vyombo vya habari vyote—vya ndani na nje—kuacha kuingilia uchunguzi unaoendelea wa Tume Huru ya Uchunguzi iliyoanzishwa na Rais, akisema kuwa kama kuna chombo chochote cha habari chenye taarifa linazodai kuwa za kiuchunguzi, kinapaswa kuwasilisha ushahidi wake kwa tume hiyo ili ufuatiliwe kisheria.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutetea uhuru wa vyombo vya habari, lakini uhuru huo lazima uende sambamba na misingi ya weledi, ukweli na uwajibikaji kwa maslahi ya taifa.

Leave A Reply