
Magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo yanaongezeka nchini Tanzania, yakichangia takribani asilimia 34 ya vifo vyote. Hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuongeza juhudi za kinga, uchunguzi wa mapema na utoaji wa elimu ya afya kwa jamii.
Kutokana na hali hiyo, Vodacom Tanzania Foundation imeanzisha kambi ya afya bure kwa wakazi wa Morogoro, ikilenga kutoa huduma za uchunguzi na ushauri wa kitaalamu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza. Kambi hiyo inafanyika kuanzia tarehe 10 hadi 13 Machi 2026 katika viwanja vya Shule ya Kilosa Mjini, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kupitia ushirikiano na madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, huduma zinazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na uchunguzi wa shinikizo la damu, kisukari na ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, amesema kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya jamii, hivyo taasisi hiyo itaendelea kusaidia upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, aliishukuru Vodacom Tanzania Foundation pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hasa katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma. Alisema kambi hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wakazi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Sandra Oswald alisema kuwa lengo la kambi hizo ni kuwahamasisha wananchi kufanya uchunguzi wa afya mapema ili kuepuka madhara makubwa ya magonjwa yasiyoambukiza. Aliongeza kuwa Vodacom Tanzania Foundation itaendelea kushirikiana na wataalamu wa afya na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za kinga na uchunguzi zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan wenye changamoto za kifedha au walioko mbali na vituo vya afya.
Mpango huo pia unaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Kimataifa (SDG 3) yanayolenga kuhakikisha afya bora na ustawi kwa wote. Vodacom Tanzania Foundation imewahimiza wakazi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika kambi hiyo ili kufanyiwa uchunguzi na kupata elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, kwani uchunguzi wa mapema ni hatua muhimu katika kujenga jamii yenye afya bora.
