×

Minara ya Mawasiliano Yazinduliwa, Rais Samia Ahimiza Ubunifu (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Tuzo Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao kutoka Kampuni ya Vodacom Tanzania Andrew Lupembe kwenye hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma tarehe 10 Aprili, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewahimiza wadau mbalimbali nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha ubunifu, kuongeza uwekezaji na kupanua miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na maendeleo ya kidigitali.

Akizungumza Ijumaa, Aprili 10, 2026 wakati wa uzinduzi wa minara 758 ya mawasiliano pamoja na maunganisho ya Mkongo wa Taifa katika wilaya 85, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, Rais Samia amesema maendeleo ya kidigitali yanahitaji ushirikiano wa sekta zote.

Amesema Serikali inaendelea kupanua huduma za mawasiliano ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari ya kuelekea uchumi wa kidigitali jumuishi.

“Naomba kuwahimiza wadau wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza ubunifu, kukuza uwekezaji na kupanua miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari yetu kuelekea Tanzania ya uchumi wa kidigitali na jumuishi,” amesema Rais Samia.

Aidha, ameongeza kuwa upanuzi wa huduma za mawasiliano vijijini na maeneo ya pembezoni unatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta muhimu ikiwemo elimu, afya na biashara mtandao, hatua inayolenga kuimarisha maendeleo jumuishi nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla akisaini Hati ya Makabidhiano kati ya Serikali na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yas Tanzania Bw. Pierre Canton-Bacara (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Bw. Charles Kamoto wa kwanza (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao wa Kampuni ya Vodacom Tanzania Bw. Andrew Lupembe katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma tarehe 10 Aprili, 2026
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya wadau wa Sekta ya Mawasiliano katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma kabla ya Uzinduzi wa minara 758, maunganisho ya Mkongo wa Mawasiliano katika Wilaya 85 na kukabidhi Mkongo wa Mawasiliano Serikalini, tarehe 10 Aprili, 2026.

Leave a Comment