×

Rais Samia Atoa Ujumbe Mkali Kuhusu Mustakabali wa Demokrasia Nchini – Video

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema demokrasia ya kweli haiwezi kunakiliwa kutoka mataifa mengine bila kuzingatia mazingira ya ndani, akisisitiza kuwa lazima ijengwe kwa kuzingatia mila, desturi na utamaduni wa nchi husika.

Akizungumza Aprili 23, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alinukuu kauli ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere, aliyewahi kusema kuwa “Demokrasia si chupa ya Soda ambayo unaweza kuiagiza,” akimaanisha kuwa mfumo huo unapaswa kukua kulingana na uhalisia wa jamii.

Rais Samia alieleza kuwa tangu Uhuru na hasa baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania imekuwa ikijenga demokrasia yake kwa misingi yake yenyewe. Alitaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa chini ya falsafa ya 4R, ikiwemo majadiliano na wadau wa siasa, marekebisho ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa, pamoja na kupanua wigo wa uhuru wa vyombo vya habari.

Aidha, alizungumzia taarifa zilizokuwa zikisambazwa kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025, akisema baadhi zilikuwa na upotoshaji, lakini sasa ukweli umewekwa wazi kupitia ripoti ya Tume ya uchunguzi iliyofanya kazi kwa weledi na kutumia takwimu sahihi.

Rais Samia pia aliahidi kuwa Serikali itaendelea kufuatilia madai ya wananchi waliopoteza ndugu zao wakati wa vurugu hizo ili kuhakikisha ukweli wote unajulikana na hatua stahiki zinachukuliwa.

Katika hotuba yake, alitoa wito kwa Watanzania kulinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa ni rahisi kuharibu lakini ni vigumu kujenga upya. Alionya dhidi ya kuchochewa kufanya vurugu, akisema hatua hizo huongeza matatizo badala ya kuyatatua.

Akihitimisha, Rais Samia alisisitiza kuwa bado anasimamia misingi ile ile ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi upya), na akaomba ushirikiano wa wananchi wote katika kuhakikisha taifa linaendelea mbele kwa umoja na mshikamano.

Leave a Comment