
Marekani imeendelea kusisitiza kuwa bado iko tayari kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran iwapo makubaliano ya kusitisha mapigano yatavunjika.
Akizungumza katika taarifa ya Pentagon, Mkuu wa Majeshi wa Marekani, Dan Caine, alisema vikosi vya Marekani vimejipanga kikamilifu na viko katika hali ya utayari wa kurejea kwenye operesheni za kijeshi wakati wowote ikihitajika.
Caine alieleza kuwa Marekani inaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya meli zinazopita katika maeneo yanayohusiana na Iran, ikiwa ni sehemu ya hatua za kudhibiti usafirishaji baharini.
Kwa mujibu wake, hadi asubuhi ya leo Aprili 24, 2026 meli 34 zimezuiwa na kurejea nyuma baada ya kukutana na vikosi vya Marekani katika maeneo ya ukaguzi wa baharini.

Hata hivyo, meli moja inayoitwa Touska haikuzingatia maelekezo ya kusimama, hatua iliyosababisha kuingiliwa kwa nguvu na majeshi ya Marekani. Caine amesema meli hiyo ilipuuza maonyo kwa muda wa takribani saa sita, na baadaye ilifyatuliwa risasi za onyo kabla ya hatua ya kuharibu injini yake kuruhusiwa ili kuizuia kuendelea na safari.
Baada ya tukio hilo, meli hiyo ilikamatwa na vikosi maalum vya Marekani, na sasa meli pamoja na wahudumu wake wapo chini ya ulinzi wa Marekani.
Caine alisisitiza kuwa operesheni hizo zinaendelea kwa lengo la kuhakikisha usalama wa njia za baharini na utekelezaji wa zuio dhidi ya shughuli zinazohusiana na Iran.