×

Mgogoro wa Iran Waibua Mpasuko Ndani ya NATO, Hispania na Marekani Zapishana

Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez

Mvutano umeibuka ndani ya NATO baada ya taarifa kudai kuwa Marekani inaweza kufikiria kuchukua hatua dhidi ya Hispania kufuatia msimamo wake kuhusu vita ya Iran.

Hata hivyo, NATO imeweka wazi kuwa haina mamlaka ya kusimamisha au kufukuza nchi mwanachama, ikieleza kuwa mkataba wake wa kuanzishwa haujatoa nafasi ya hatua kama hiyo.

Kauli hiyo imekuja kufuatia ripoti iliyodai kuwa barua pepe ya ndani ya Pentagon ilipendekeza njia za kuwaadhibu washirika wanaodaiwa kushindwa kuunga mkono kikamilifu juhudi za Marekani katika mzozo huo.

Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, amepuuza taarifa hizo akisema serikali yake haifanyi kazi kwa misingi ya taarifa zisizo rasmi. Amesisitiza kuwa Hispania inaendelea kushirikiana na washirika wake lakini ndani ya mipaka ya sheria za kimataifa.

Kwa upande wake, Donald Trump ameendelea kuwakosoa washirika wa NATO kwa kile anachodai kuwa ni kushindwa kubeba wajibu wao, akisisitiza kuwa Marekani imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa usalama wa muungano huo.

Donald Trum akiwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer walipokutana.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amesema kuongezeka kwa ushiriki wao katika vita hiyo si kwa maslahi ya taifa hilo, licha ya kuruhusu matumizi ya baadhi ya vituo vya kijeshi na kushiriki katika operesheni za anga.

Ripoti hiyo pia iligusia uwezekano wa Marekani kupitia upya msimamo wake kuhusu Kisiwa cha Falkland, eneo ambalo limekuwa chanzo cha mvutano wa muda mrefu kati ya Uingereza na Argentina tangu vita ya Falklands.

Licha ya mvutano huo, viongozi mbalimbali wa Ulaya wameendelea kusisitiza umuhimu wa umoja ndani ya NATO, wakionya kuwa migawanyiko inaweza kudhoofisha nguvu ya muungano huo katika kukabiliana na changamoto za kiusalama duniani.

MAHANDAKI SITA ya SIRI YAGUNDULIWA MWANZA – POLISI WAWAKAMATA WATU WATATU PAPO HAPO..

Leave a Comment