×

Bahati ya ‘Mwaka Umenyooka’ Yabadilisha Maisha ya Mwalimu Hai Sekondari

Mwalimu Geofrey Pascal Paul wa Shule ya Sekondari Hai mkoani Kilimanjaro ameibuka mshindi wa gari aina ya Mazda CX5 kupitia kampeni ya “Mwaka Umenyooka” inayoratibiwa na My Airtel App, na hivyo kubadilisha kwa kiasi kikubwa maisha yake ya kila siku.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa gari hilo iliyoandaliwa na Airtel Tanzania, Mwalimu Paul alisema ushindi huo ni hatua kubwa kwake, hasa katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake ya kikazi. Alieleza kuwa awali alikuwa akitegemea usafiri wa pikipiki kwenda na kurudi shule, hali iliyokuwa ikimpa changamoto hasa nyakati za mvua, lakini sasa ana uhakika wa usafiri salama na wa uhakika zaidi.

Mwalimu Paul alifafanua kuwa hakutarajia kabisa kupata ushindi huo, kwani aliingia kwenye droo hiyo bila kujua baada ya kufanya muamala wa kawaida kupitia Airtel Money App. Alituma shilingi 100,000 kwa ajili ya matibabu ya baba yake, jambo lililomuingiza moja kwa moja kwenye droo ya kampeni hiyo.

“Sikuwahi kufikiria kuwa siku moja ningeweza kumiliki gari la kisasa kama hili. Kwangu hii ni kama ndoto. Mungu ameniona kupitia My Airtel App. Nilifanya muamala wa laki moja tu kwa ajili ya kusaidia mgonjwa, lakini umeleta baraka kubwa. Ninamshukuru sana Airtel kwa kuwajali wateja wao,” alisema Mwalimu Paul kwa furaha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Airtel Money wa Airtel Tanzania, Andrew Rugamba, alisema kampeni hiyo inalenga kurudisha kwa jamii pamoja na kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha kidigitali. Aliongeza kuwa kupitia Airtel Money App, Watanzania wanaweza kufanya miamala mbalimbali kwa urahisi zaidi huku wakichangia kukuza uchumi wa kidigitali nchini.

 

Leave a Comment