
Kiungo mshambuliaji, Matheus Cunha ameendelea kumiminia sifa kocha wa muda wa Manchester United, Michael Carrick, akisema anastahili kupewa kibarua cha kudumu kutokana na matokeo na mchango wake mkubwa ndani ya klabu hiyo.
Carrick, ambaye aliwahi kuwa kiungo tegemeo wa Manchester United kwa zaidi ya mechi 400 akiwa mchezaji, amerudi Old Trafford kama kocha na ameonekana kuibadilisha timu hiyo kwa kasi kubwa ya matokeo mazuri.
Tangu alipokabidhiwa majukumu ya muda mwezi Januari, Carrick ameiongoza United katika mechi 14, akishinda 10 kati yake, ikiwa ni pamoja na ushindi muhimu dhidi ya wapinzani wakubwa kama Arsenal, Manchester City na Chelsea. Ushindi huo umeiwezesha United kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2023/24.
Akizungumza baada ya mechi, Cunha alisema wazi kuwa Carrick anafaa kubaki Old Trafford kwa kudumu kutokana na namna anavyowahamasisha wachezaji na kuwapa mbinu za kisasa za soka.

“Kwa kweli, nadhani anastahili nafasi hiyo. Kile anachokifanya hapa kinatupa ujasiri mkubwa. Nimeanza benchi chini yake lakini jinsi anavyotufundisha ni ya kipekee. Ana kitu cha kipekee, kama ilivyokuwa enzi za Sir Alex Ferguson,” alisema Cunha.
Aliongeza kuwa Carrick ana uwezo wa kuwafundisha wachezaji kuelewa soka la kiwango cha juu na kuwajenga kiakili na kimchezo, jambo linaloifanya timu kucheza kwa ufanisi zaidi.
Wachezaji wengine pia wamekuwa wakimpa sapoti Carrick, ambapo Amad Diallo aliwahi kusema kuwa yeye ndiye “kocha sahihi kwa kazi hiyo,” huku Harry Maguire akieleza kuwa Carrick anapaswa kuwa “miongoni mwa wanaopigiwa hesabu kwa nafasi ya kudumu.”
Mbali na hilo, Cunha pia alizungumzia kuhusu mustakabali wa kiungo mkongwe Casemiro, akidokeza kuwa bado kuna uwezekano wa kubaki Old Trafford licha ya taarifa za awali za klabu kumaliza mkataba wake.
“Unajua, huwezi kujua. Casemiro ni mchezaji muhimu sana na mtu mzuri pia. Ni fahari kuwa naye timu moja,” alisema Cunha.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya klabu zinaonyesha kuwa Manchester United bado ina mpango wa kuachana na Casemiro ili kufanya maboresho katika eneo la kiungo kuelekea msimu ujao.
Mustakabali wa Carrick sasa unaendelea kuwa mada kubwa Old Trafford, huku wachezaji na mashabiki wengi wakionekana kuunga mkono azma ya kocha huyo kubaki kwa muda mrefu klabuni hapo.