×

Rais Samia Amteua Drogba Kuwa Balozi wa Tanzania Kuelekea AFCON 2027

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na mshambuliaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast na klabu ya Chelsea FC, Didier Drogba, katika Ikulu ya Ikulu Chamwino leo Mei 5, 2026.

Katika mazungumzo yao, Rais Samia amemuomba nyota huyo wa soka kuwa Balozi wa Tanzania kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2027, hatua inayolenga kuongeza hamasa ya michezo na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia soka.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mshambuliaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast na Timu ya Chelsea ya Uingereza Didier Drogba mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Aidha, Rais Samia ameielekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na Drogba ili kubadilishana uzoefu katika kuanzisha na kuendesha vituo vya kukuza vipaji vya michezo (Sports Academy), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha maendeleo ya soka na michezo kwa ujumla nchini.

Kwa upande wake, Drogba amemshukuru Rais Samia kwa mwaliko huo na kuonesha utayari wake wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza michezo na vipaji vya vijana.

Mbali na mafanikio yake makubwa ndani ya uwanja wa soka, Drogba anatambulika pia kwa mchango wake wa kijamii, ikiwemo juhudi zake mwaka 2005 zilizosaidia kusitishwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast, hatua iliyomjengea heshima kubwa kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mshambuliaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast na Timu ya Chelsea ya Uingereza Didier Drogba mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, tarehe 05 Mei, 2026.

Leave a Comment