
Mbunge wa Buchosa Eric Shigongo ameibua tena bungeni changamoto ya wananchi wa jimbo lake kushambuliwa na mamba wanapokuwa wakifanya shughuli zao za kila siku katika maeneo ya Ziwa Victoria.
Akichangia bungeni jijini Dodoma, Shigongo amesema idadi ya mamba imeongezeka kwa kiwango kikubwa hali inayohatarisha maisha ya wananchi, hasa wavuvi na wakazi wanaotegemea shughuli za ziwani kujipatia kipato.
Mbunge huyo amesema serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka ikiwemo kuanza kuwavuna baadhi ya mamba hao ili kulinda maisha ya wananchi.
“Maisha ya binadamu ni muhimu kuliko mamba. Wananchi wetu wanaendelea kupoteza maisha wakiwa wanatafuta riziki zao,” amesema Shigongo bungeni.
Katika hoja nyingine, Shigongo amehoji sababu za wananchi wa Buchosa kutozwa fedha wanapopita katika Hifadhi ya Kome kuelekea kwenye shughuli zao za kila siku.
Amesema tayari amewasilisha malalamiko hayo kwenye wizara husika na kuitaka serikali kufanya marekebisho ya sheria inayosababisha wananchi kubebeshwa tozo hizo, ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, wananchi wanaona tozo hizo ni mzigo kwao kwani maeneo hayo ni sehemu wanazopita mara kwa mara kwa shughuli za uvuvi, biashara na maisha ya kawaida.