×

Muhoozi Ataka Rolls Royce Ya Spika wa Bunge Iuzwe Kwa Mnada

Spika wa zamani wa Bunge la Uganda, Anita Among

Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Muhoozi Kainerugaba, amesema anataka gari la kifahari aina ya Rolls Royce Cullinan linalodaiwa kumilikiwa na aliyekuwa Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among, liuzwe kwa mnada na fedha zake kurejeshwa serikalini.

Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa X Mei 19, 2026, Muhoozi alisema gari hilo lenye thamani inayokadiriwa kufikia dola 400,000 za Marekani (Tsh 104,,3537,600) ni sehemu ya mali zinazochunguzwa katika tuhuma za rushwa zinazomkabili Anita Among.

“Tumelichukua lile Rolls Royce, sasa liko mikononi mwetu. Tunaweza kuliuza kwa mnada na fedha zitakazopatikana zirudi kusaidia Serikali,” amesema Muhoozi.

Sakata hilo lilianza kushika kasi Mei 16, 2026 baada ya nyumba ya Anita Among kuanza kufanyiwa upekuzi muda mfupi baada ya kumaliza muhula wake wa kwanza kama Spika wa Bunge la Uganda. Pia alitakiwa kusitisha mpango wake wa kuwania muhula mwingine wa uongozi.

Mei 17, Among alitangaza kuwa hatawania tena nafasi hiyo na kwamba yuko tayari kushirikiana na vyombo vya uchunguzi ili kubaini ukweli kuhusu chanzo cha utajiri wake.

Siku moja baadaye, Mei 18, vyombo vya usalama vilikamata magari kadhaa yanayodaiwa kumilikiwa na Among, likiwemo Rolls Royce Cullinan iliyozua mjadala mkubwa nchini Uganda kutokana na thamani yake kubwa.

Muhoozi Kainerugaba

Wananchi wengi wa Uganda wamekuwa wakijiuliza namna mtumishi wa umma anaweza kumiliki gari la kifahari la thamani kubwa kiasi hicho, huku wakitaka uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu chanzo cha fedha zilizotumika kulinunua.

Muhoozi amesema hata yeye, licha ya kuwa Mkuu wa Majeshi na mtoto wa Rais wa Uganda, hajawahi kutumia gari la thamani kama hiyo, kauli iliyozidi kuchochea mjadala mkubwa nchini humo.

Leave a Comment