
Rais wa Marekani Donald Trump amesema amepewa dhamana kutoka Iran kwamba taifa hilo halitatengeneza silaha za nyuklia, huku taarifa zikieleza kuwa ametuma pendekezo jipya lenye masharti makali zaidi kwa Iran ili kufanikisha makubaliano ya amani.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka vyombo vya habari vya Marekani, pendekezo hilo jipya linaweza kuchelewesha zaidi kufikiwa kwa makubaliano rasmi ya kumaliza mvutano wa Mashariki ya Kati pamoja na kufunguliwa kwa njia muhimu ya bahari ya Hormuz ambayo imeathiri biashara ya mafuta duniani.
Akizungumza katika mahojiano na mkwe wake Lara Trump kupitia Fox News, Trump alisema kipaumbele chake kikubwa ni kuhakikisha Iran haimiliki silaha za nyuklia.
“Kitu pekee ninachohitaji kuhakikishiwa ni kutokuwepo kwa silaha za nyuklia. Wamekubali hilo,” alisema Trump.

Hata hivyo, Iran imeendelea kuonesha mashaka kuhusu kauli za Trump, huku ikisisitiza kuwa bado hakuna makubaliano ya mwisho yaliyofikiwa. Serikali ya Iran pia inataka dola bilioni 12 (TSh trilioni 31.2) zilizoshikiliwa na Marekani kabla ya mazungumzo kuingia hatua ya kina kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Spika wa Bunge la Iran Mohammad Bagher Qalibaf amesema Iran haitategemea ahadi za Marekani pekee bali itahitaji kuona hatua halisi zikichukuliwa.

Mvutano huo umeendelea licha ya kuwepo kwa usitishaji wa mapigano wa muda kati ya Marekani na Iran uliokubaliwa mwezi Aprili. Wiki hii kuliripotiwa mashambulizi mapya baada ya vikosi vya Marekani kushambulia bandari ya Bandar Abbas na Iran kujibu kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amesema Marekani ipo tayari kurejea vitani ikiwa mazungumzo yatashindikana.
Iran pia imeendelea kusisitiza kuwa itadhibiti kikamilifu Mlango wa Hormuz, huku wabunge wake wakitarajiwa kupitisha mpango mpya wa usimamizi wa eneo hilo muhimu kwa biashara ya kimataifa ya mafuta.