×

Marekani Yapanga Kutumia Mali za Iran Kufidia Uharibifu Mashariki ya Kati

Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent akiongea mbele ya wabunge katika Capitol Hill, Washington DC, Juni 4, 2026.

Serikali ya Marekani inapanga kuangalia uwezekano wa kuelekeza mali za Iran kwenda mataifa ya Ghuba kwa ajili ya kugharamia ukarabati na fidia ya uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Iran.

Mataifa ya Ghuba ni nchi zilizopo katika eneo la Ghuba ya Uajemi (Persian Gulf) Mashariki ya Kati Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Kuwait, Bahrain, Oman

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Iran kufanya mashambulizi dhidi ya Kuwait na Bahrain, huku Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, akitoa maagizo kwa timu maalum kufanya tathmini ya gharama za uharibifu uliosababishwa kwa washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba.

Chanzo hicho kilisema Marekani pia inatafakari kutumia baadhi ya mali za Iran zilizozuiliwa au nyingine zinazohusishwa na taifa hilo kufidia gharama za ukarabati huo.

Picha iliyotolewa na vyombo vya habari vya serikali nchini Kuwait ikionyesha maafisa wakikagua uharibifu katika moja ya Uwanja wa ndege.

Kauli hiyo imekuja baada ya mshauri wa kiongozi mkuu wa Iran, Mohsen Rezaei, kuiambia CNN kwamba makubaliano ya amani yanaweza kufikiwa iwapo Marekani itaachia dola bilioni 24 za mali za Iran zilizogandishwa.

Wakati huo huo, mazungumzo ya amani yanaonekana kusuasua licha ya Pakistan kutuma ujumbe maalum Tehran kwa ajili ya kuwasilisha barua kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei.

Mvutano huo umeendelea huku Marekani ikifanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya rada za pwani za Iran katika Goruk na Kisiwa cha Qeshm baada ya kudai kudungua ndege zisizo na rubani zilizotumwa na Iran katika eneo la Strait of Hormuz.

Iran kupitia Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ilisema ilijibu kwa kushambulia vituo vya Marekani nchini Kuwait na Bahrain kwa makombora ya ballistic. Jeshi la Kuwait lilisema lilidungua makombora saba yaliyopita juu ya maeneo ya makazi na kusababisha uharibifu wa mali lakini hakuna vifo vilivyoripotiwa.

Al Jubail, Saudi Arabia

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran bado ina sehemu ya uwezo wake wa makombora na ndege zisizo na rubani licha ya mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya viwanda vyake vya kijeshi.

Katika kipindi cha vita vilivyoanza Februari 28 baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran, Tehran imekuwa ikishambulia mataifa ya Ghuba yanayohifadhi vituo vya kijeshi vya Marekani pamoja na kuathiri usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz.

Ripoti zinaeleza kuwa zaidi ya makombora na drones 6,400 yalirushwa kuelekea mataifa ya Kiarabu kati ya Februari na Aprili, hali iliyosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, viwanja vya ndege, bandari, vituo vya nishati na maeneo ya kiraia.

Miongoni mwa matukio makubwa ni shambulio la drone lililolenga kituo cha nyuklia cha Barakah nchini UAE Mei 17, ambapo Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, alisema tukio hilo lilihatarisha usalama wa nyuklia licha ya kutokuwepo kwa uvujaji wa mionzi.

Mataifa kama Kuwait, UAE, Qatar, Saudi Arabia na Bahrain yameripoti uharibifu wa miundombinu ya kijeshi, viwanja vya ndege, vituo vya mafuta na maeneo ya kiraia kutokana na mashambulizi hayo ya Iran.

Wachambuzi wa kijeshi wanasema UAE na Kuwait zilitumia karibu robo tatu ya makombora yao ya kujihami aina ya Patriot wakati wa vita hivyo, jambo lililoonyesha mzigo mkubwa wa kifedha na kiusalama uliosababishwa na mzozo huo.

Leave a Comment