
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema majeshi ya nchi hiyo yataendelea kuwepo katika maeneo ya Lebanon, Syria na Gaza kwa muda usio na kikomo, licha ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran ya kusitisha vita vya Mashariki ya Kati.
Katika taarifa yake, Katz alisema serikali ya Israel chini ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imeweka mkakati wa kuhakikisha Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linaendelea kubaki katika maeneo inayoyataja kuwa ya usalama ili kulinda mipaka ya taifa hilo na wananchi wake dhidi ya vitisho vya makundi yenye msimamo mkali.
“Netanyahu na mimi tunafuata sera wazi ambapo IDF itaendelea kuwepo katika maeneo ya usalama nchini Lebanon, Syria na Gaza kwa muda usio na kikomo ili kulinda mipaka na jamii za Israel dhidi ya makundi ya kijihadi,” alisema Katz.
Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya Marekani na Iran kutangaza makubaliano ya kusitisha mapigano katika eneo la Mashariki ya Kati, hatua inayotarajiwa kupunguza mvutano uliodumu kwa miezi kadhaa.
Hata hivyo, Katz alisisitiza kuwa Israel itaendelea kuchukua hatua kali za kijeshi ikiwa itahisi usalama wake unatishiwa. Aidha, alitoa onyo kali kwa Iran, akisema kuwa shambulio lolote dhidi ya Israel litajibiwa kwa nguvu kubwa.
“Iwapo Iran itachagua kushambulia Israel kutokana na operesheni zetu nchini Lebanon, tutajibu kwa nguvu kamili,” alionya.
Tamko hilo linaashiria kuwa licha ya juhudi za kidiplomasia za kusitisha mapigano, Israel bado inaendelea kushikilia msimamo wake wa kuhakikisha usalama wa taifa hilo kupitia uwepo wa kijeshi katika maeneo yenye migogoro.
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaona kauli hiyo kama ishara kwamba changamoto za usalama katika Mashariki ya Kati bado zinaweza kuendelea hata baada ya makubaliano ya amani kati ya Washington na Tehran.