
Watanzania wanaotafuta ajira wamepata fursa mpya baada ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (PSRS) kutangaza nafasi 95 za kazi katika kada mbalimbali za afya, uhasibu na ukaguzi wa ndani.
Katika tangazo hilo, nafasi nyingi zimeelekezwa kwenye sekta ya afya ambapo zimetengwa nafasi 10 kwa Mteknolojia Msaidizi wa Maabara, nafasi 10 za Mteknolojia Msaidizi wa Dawa, nafasi 10 za Mteknolojia Msaidizi wa Radiolojia, nafasi 10 za Mteknolojia wa Radiografia, nafasi 10 za Tabibu wa Kinywa na Meno pamoja na nafasi 10 za Madaktari wa Upasuaji wa Kinywa na Meno.
Aidha, Sekretarieti hiyo imetangaza nafasi 15 za Mkaguzi wa Ndani Daraja la II na nafasi 10 za Mhasibu Daraja la II kwa wahitimu wenye sifa zinazotakiwa pamoja na vyeti vya kitaaluma vinavyotambuliwa na mamlaka husika.
Waombaji wa kada za afya wanatakiwa kuwa na usajili kutoka kwenye mabaraza ya taaluma zao, huku kada za uhasibu na ukaguzi zikihitaji waombaji kuwa na cheti cha CPA(T) au sifa nyingine zinazotambuliwa na NBAA.
Tangazo hilo linatoa fursa kwa vijana na wataalamu wenye sifa stahiki kujiunga na Utumishi wa Umma na kuchangia maendeleo ya sekta mbalimbali nchini.
Waombaji wametakiwa kuwasilisha maombi yao kupitia mfumo rasmi wa ajira wa Serikali ndani ya muda uliopangwa.