
Nyota wa vipindi vya Televisheni na mjasiriamali, Kim Kardashian, anaendelea kuishi maisha ya kifahari yanayoakisi utajiri wake unaokadiriwa kufikia dola bilioni 1.9 za Marekani sawa na trilioni 4.99 za Tanzania.
Miongoni mwa mali zake zinazovutia zaidi ni ndege yake binafsi aina ya Gulfstream G650ER yenye thamani ya takribani dola milioni 150 (Shilingi bilioni 394.05 za Tanzani) pamoja na jumba lake la kifahari lililopo Hidden Hills, California.
Aidha, Kim anamiliki mkusanyiko wa magari ya kifahari unaojumuisha magari ya Rolls-Royce yaliyobinafsishwa, Mercedes-Maybach pamoja na Lamborghini Urus.

Mbali na magari, Kim pia amekuwa akiwekeza katika sekta ya nyumba na ardhi, akiwa amewahi kumiliki mali mbalimbali za thamani kubwa katika maeneo tofauti ya California.
Vito vya thamani navyo ni sehemu muhimu ya utajiri wake. Inaripotiwa kuwa anamiliki vipande adimu vya vito vya almasi kutoka Cartier na mbunifu maarufu Lorraine Schwartz, vyenye thamani ya mamilioni ya dola. Pia ana mkusanyiko wa saa za kifahari kutoka Rolex, Patek Philippe na Audemars Piguet.

Katika upande wa mitindo, Kim anatajwa kumiliki baadhi ya mikoba adimu zaidi duniani ikiwemo Hermès Himalayan Birkin, ambayo baadhi yake huuzwa kwa mamia ya maelfu ya dola.
Sehemu kubwa ya mafanikio hayo ya kifedha imechangiwa na kampuni yake ya mavazi ya ndani na mitindo, SKIMS, ambayo imekuwa moja ya biashara zilizomuingizia mapato makubwa katika miaka ya karibuni. Mbali na biashara hiyo, Kim ameendelea kunufaika kupitia matangazo ya kibiashara, vipindi vya televisheni na uwekezaji mbalimbali, jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa wanawake matajiri zaidi katika sekta ya burudani duniani.
