
Morogoro, Juni 2026 –Kampuni ya Mawasiliano ya Yas, imesema inaendelea kujivunia kuwa sehemu ya wadau wanaounga mkono mbio za TCB Selous Marathon, tukio ambalo limeendelea kujijengea nafasi kama jukwaa muhimu la kuhamasisha afya, kukuza utalii na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, aliwapongeza waandaaji na wadau mbalimbali wanaoendelea kuunga mkono mbio hizo akisema matukio ya aina hiyo yana mchango mkubwa katika kukuza michezo, afya, utalii na uchumi wa nchi.

“Serikali inaendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika michezo kwa sababu ni nyenzo muhimu ya kujenga taifa lenye afya na nguvu kazi yenye tija.
Tunawapongeza waandaaji wa TCB Selous Marathon pamoja na wadau kama Yas na Mixx kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya jamii kupitia michezo.
Matukio haya yanasaidia pia kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya utalii ndani na nje ya nchi,” alisema Mwinjuma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kusini, Bw. Joseph Mutalemwa, alisema ushiriki wa kampuni hiyo katika mbio hizo unaakisi dhamira yake ya kuunga mkono mipango inayowaleta watanzania pamoja na kuleta matokeo chanya katika jamii.
Alisema mbio hizo zimekuwa zaidi ya mashindano ya riadha kwa kuwa inachangia kuitangaza Morogoro na vivutio vyake vya utalii, huku ikifungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi na wafanyabiashara wanaonufaika na shughuli zinazozunguka tukio hilo.
“Tunafurahi kuwa sehemu ya tukio hili ambalo si tu linahamasisha afya na ustawi wa jamii, bali pia linasaidia kuitangaza Morogoro kama kitovu cha utalii na shughuli za kiuchumi,” alisema Mutalemwa.
Kwa mujibu wake, Yas na Mixx zinaamini michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga afya bora, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuhamasisha maendeleo endelevu katika jamii.
Aidha, Mutalemwa alisema Yas imeendelea kuwekeza katika kuimarisha huduma za mawasiliano nchini kupitia uwekezaji wa zaidi ya shilingi trilioni moja katika miundombinu ya kidijitali, hatua inayowezesha wananchi kuwasiliana, kufanya biashara na kupata huduma mbalimbali kwa urahisi zaidi.
Alibainisha kuwa kampuni hiyo kwa sasa ina zaidi ya minara 4,800 nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuhakikisha huduma bora za mawasiliano zinapatikana katika maeneo mengi zaidi ya Tanzania.
Sambamba na hilo, alisema huduma za kifedha za Mixx zinaendelea kuwawezesha Watanzania kufanya miamala kwa usalama, haraka na kwa urahisi, jambo linalochangia kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na matumizi ya huduma za kidijitali.
Kwa upande wake, mshiriki wa mbio hizo, Janeyah Mkwizu, alisema TCB Selous Marathon imeendelea kuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi huku ikihamasisha afya na kuitangaza Morogoro kama moja ya maeneo muhimu ya utalii nchini.
“Mbio hizi zimekuwa zaidi ya mashindano. Zinatuleta pamoja kama jamii, zinatuhamasisha kuzingatia afya zetu na wakati huo huo zinaitangaza Morogoro kwa watu wengi zaidi.
Tunawashukuru wadau kama Yas na Mixx ambao wanaendelea kuunga mkono matukio kama haya yenye manufaa kwa jamii,” alisema Mkwizu.