Waokoaji wanapekua vifusi watafuta walionusurika matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyokumba maeneo ya karibu na mji mkuu wa Venezuela na kusababisha vifo vya takribani watu 235 na kuwajeruhi zaidi ya 1,500.
Katika Caracas na mji wa karibu wa pwani wa La Guaira, watu walisikika wakiomba msaada kutoka chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.
Tetemeko la kwanza la ukubwa wa 7.2 lilifuatiwa sekunde chache baadaye na lingine lenye nguvu zaidi ya 7.5, kulingana na Utafiti wa Jiolojia wa Marekani (USGS), na kusababisha uharibifu mkubwa zaidi.
Watu wengi zaidi wanahofiwa kufariki, huku wengine wakiwa wameachwa bila makao au kulala barabarani kwa kuogopa kurejea kwenye majengo yaliyoharibiwa baada ya mkasa huo.
Matetemeko ya ardhi yalitokea saa kumi na mbili na dakika ne kwa saa za ndani(22:04 GMT) siku ya Jumatano – sikukuu ya kitaifa nchini Venezuela, kumaanisha kuwa watu walikuwa nyumbani ikilinganishwa na siku ya kawaida ya juma.
Siku ya Alhamisi Rais wa Bunge la Venezuela Jorge Rodríguez, aliripoti kwamba idadi ya waliofariki imeongezeka, baada ya Rais wa mpito wa nchi hiyo Delcy Rodríguez kutangaza hali ya dharura.
Nchi kadhaa zimeahidi kusaidia juhudi za uokoaji, huku Marekani ikiahidi msaada wa dola milioni 150. Jeshi la Marekani linatuma meli za usafiri na ndege kusaidia shughuli ya uokoaji na “operesheni za msaada wadharura”, ilisema katika taarifa.
Jorge Rodríguez alisema majengo 250 yameharibiwa au kupotea, hasa La Guaira, ambapo BBC ilithibitisha picha za hoteli ya ghorofa 10 iliyoharibiwa na kuwa vifusi. Siku ya Alhamisi, watu walikuwa wakitafuta wapendwa huko.
Juan Ortiz ameiambia BBC kwamba mmoja wa marafiki zake wa karibu amethibitishwa kufariki, mwingine anaaminika kuwa chini ya vifusi, na takribani watu 20 anaowafahamu wanaoishi katika eneo la pwani hawajulikani waliko.
“Ninakabiliwa na mshtuko na kuchanganyikiwa, nasikitika kwamba siwezi kusaidia,” mwanafunzi wa matibabu mjini Caracas alisema.