
NEW YORK – Maandalizi ya sherehe inayodaiwa kuwa ya harusi ya mastaa wa Marekani, Taylor Swift na Travis Kelce, imeripotiwa kuanza katika ukumbi wa Madison Square Garden (MSG), New York City, huku dalili mbalimbali zikionekana ndani na nje ya eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani, vifaa mbalimbali vimeanza kuingizwa katika ukumbi huo, ikiwemo maboksi yaliyoandikwa “Garden Party” na “Mirror Ball”, pamoja na maandalizi ya zulia jekundu (red carpet) yaliyoshuhudiwa katika maeneo ya kuingilia ukumbini.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa zaidi ya wafanyakazi 40 wa MSG wamekuwa wakifanya kazi usiku kucha kuandaa ukumbi huo kwa ajili ya tukio kubwa linalotarajiwa kufanyika siku zijazo.
Pia, magari ya kubeba mizigo na vifaa vya mapambo yameripotiwa kuingia na kutoka katika eneo hilo, huku baadhi ya sehemu za ukumbi zikionekana kuwekewa mandhari ya kijani na mapambo maalum yanayohusishwa na “garden party”.

Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na maandalizi hayo, tukio hilo linatajwa kuwa linaweza kujumuisha sherehe ya awali yenye wageni takriban 100, ikifuatiwa na hafla kubwa zaidi yenye zaidi ya wageni 1,000.
Hata hivyo, bado hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa Taylor Swift, Travis Kelce au wasimamizi wao kuhusu tarehe na aina ya tukio hilo, huku taarifa nyingi zikiendelea kubaki katika kiwango cha uvumi wa vyombo vya habari.
Uvumi huo umeongeza msisimko mkubwa miongoni mwa mashabiki duniani, hasa kutokana na ukweli kuwa MSG ni moja ya kumbi kubwa na za hadhi ya juu zaidi duniani, inayotumiwa zaidi kwa matamasha makubwa na matukio ya michezo.
Endapo taarifa hizo zitathibitika, sherehe hiyo inaweza kuwa miongoni mwa harusi kubwa na za kipekee kuwahi kufanyika katika historia ya burudani Marekani.