×

Mkutano Mkuu wa 53 wa TBL Wathibitisha Mgao wa Muda kwa Wanahisa

Kushoto Ami R. Mpungwe (Mwenyekiti wa Mpito wa Bodi ya Tanzania Breweries PLC), Michelle Kilpin (Mtendaji Mkuu wa TBL) [Katikati], na Avito Swai (Mkuu wa Kitengo cha Fedha TBL) [Kulia] wakizungumza na wanahisa katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa, ambapo wanahisa wamepitisha taarifa ya fedha ya mwaka wa mapato wa 2025/2026 kufuatia ukuaji wa faida uliotangazwa hii leo.

Wanahisa wa Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL Plc) wamepitisha Ripoti ya Wakurugenzi, Ripoti ya Wakaguzi wa Hesabu pamoja na taarifa za fedha zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2025, wakati wa Mkutano Mkuu wa 53 wa Wanahisa uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, wanahisa pia walithibitisha mgao wa muda (interim dividend) uliolipwa kwa mwaka huo na kuidhinisha uteuzi wa kampuni ya PricewaterhouseCoopers (PwC) kuwa wakaguzi wa hesabu wa nje kwa mwaka wa fedha unaoishia Desemba 31, 2026.

TBL ilitangaza matokeo yenye kuonyesha ukuaji mkubwa wa biashara mwaka 2025, ambapo mapato yaliongezeka kwa asilimia 13 huku faida ya uendeshaji ikikua kwa asilimia 35. Kampuni imeeleza mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya bia na vileo vikali, usimamizi madhubuti wa gharama, uwekezaji katika chapa zake na maboresho ya mfumo wa usambazaji wa bidhaa.

Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBL, Ami R. Mpungwe, alisema Mkutano Mkuu wa Wanahisa unaendelea kuwa jukwaa muhimu la uwajibikaji na uwazi, huku ukiimarisha imani ya wanahisa na kuweka msingi wa ukuaji endelevu wa kampuni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle N. Kilpin, alisema mafanikio ya mwaka 2025 yametokana na uimara wa chapa za kampuni, utekelezaji wa mikakati kwa nidhamu na imani kubwa kutoka kwa wateja, wanahisa na wadau wengine.

Aliongeza kuwa kampuni itaendelea kuwekeza katika chapa zake, mifumo ya kidijitali, matumizi ya malighafi zinazozalishwa nchini pamoja na kuongeza ufanisi wa shughuli zake ili kuendelea kujenga thamani kwa wanahisa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Mbali na mafanikio ya kifedha, TBL imeendelea kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa ndani kupitia Kiwanda cha Kimea cha Kilimanjaro, kinachozalisha tani 8,000 za kimea kwa mwaka na kuongeza matumizi ya shayiri inayolimwa nchini. Kampuni pia imeendelea kuwaunga mkono wakulima wa shayiri na mtama, kupanua mfumo wa kidijitali wa kuagiza bidhaa na kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara wa rejareja.

Katika eneo la uendelevu, TBL imeeleza kuwa asilimia 92 ya vifungashio vyake vinaweza kurejeshwa au vinatengenezwa kwa malighafi zilizorejelewa, huku ikiendelea kuhamasisha matumizi yenye uwajibikaji ya bidhaa zake na kuchangia maendeleo ya jamii pamoja na uchumi wa Tanzania.

Leave a Comment