
Kampuni ya Airtel Tanzania imeimarisha huduma za mawasiliano katika mashindano ya Great Ruaha Marathon 2026 yaliyofanyika Julai 3 na 4 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, hatua iliyochangia uratibu mzuri wa mashindano na kuunga mkono juhudi za kukuza utalii na uhifadhi wa mazingira.
Mashindano hayo, ambayo yameendelea kujijengea umaarufu nchini, yanatumika kuhamasisha uhifadhi wa ikolojia ya Mto Mkuu Ruaha huku yakitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Kanda ya Kusini.
Airtel Tanzania, ambayo ilikuwa mdhamini rasmi wa huduma za mawasiliano, ilihakikisha waandaaji, washiriki, vikosi vya uokoaji, wanahabari na wageni wanapata huduma za mawasiliano ya uhakika katika kipindi chote cha mashindano. Kampuni hiyo pia ilishirikisha wafanyakazi wake kushiriki mbio hizo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha afya na ustawi.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Airtel Tanzania, Prosper Mafole, alisema mawasiliano ya uhakika ni sehemu muhimu ya mafanikio ya matukio makubwa yanayofanyika katika maeneo ya hifadhi na vivutio vya utalii.
“Mawasiliano yanawezesha uratibu wa shughuli zote muhimu, yanaimarisha usalama na kuwapa washiriki na wageni uzoefu bora. Tunafurahia kuwa sehemu ya juhudi zinazochanganya uhifadhi wa mazingira, utalii na maendeleo ya jamii.”
Akimwakilisha Waziri Mkuu, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema matukio ya michezo yanayofanyika katika maeneo ya utalii yana mchango mkubwa katika kuitangaza Tanzania kimataifa na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa nchi.
“Great Ruaha Marathon inaonyesha namna michezo inavyoweza kutumika kuitangaza Tanzania duniani. Matukio kama haya yanavutia watalii, yanazalisha fursa za kiuchumi kwa wananchi na kuhamasisha uhifadhi wa rasilimali za asili.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Sustainable Youth Development Partnership (SYDP), Edward Athanas, aliipongeza Airtel Tanzania kwa kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana muda wote wa mashindano.
“Mawasiliano ya uhakika yalirahisisha uratibu wa waandaaji, vikosi vya dharura na washiriki. Hilo lilichangia mashindano kufanyika kwa usalama na mafanikio.”
Great Ruaha Marathon imeendelea kukua na kuwa jukwaa muhimu linalounganisha serikali, sekta binafsi na wadau wa uhifadhi katika kulinda mazingira, kukuza utalii endelevu na kuchochea maendeleo ya uchumi wa jamii zinazozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.