×

Vodacom Foundation Yawezesha Wanawake na Vijana Kupitia Mradi wa TELS

Katika kuadhimisha Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation Sandra Oswald amesema taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mafunzo ya ujasiriamali na matumizi ya teknolojia za kifedha.

Akizungumza katika banda la TWCC, Sandra alisema kupitia ushirikiano wa Vodacom Tanzania Foundation, CEO Roundtable na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC), wanaendesha mradi wa TELS (Thinking Equal, Leading Smart) unaolenga kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo kuendesha na kukuza biashara zao.

Amesema tangu mradi huo uanze, zaidi ya washiriki 800 wamepatiwa mafunzo ya uongozi wa biashara, matumizi ya huduma za fedha kidijitali kama M-Pesa na M-Koba pamoja na mbinu za kupata fursa za kifedha na mitaji.

Sandra alieleza kuwa kwa ujumla Vodacom Tanzania Foundation imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanawake 500,000 kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji wa kiuchumi, huku pia ikishirikiana na wadau kuboresha mazingira ya sera ili kurahisisha ukuaji wa biashara ndogo na za kati.

Ameongeza kuwa katika awamu ya kwanza ya mafunzo yaliyofanyika jijini Dodoma, vijana walijengewa uwezo kuhusu misingi ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara na matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali, hatua inayolenga kuwasaidia kukuza biashara zao kwa ufanisi.

Kwa kumalizia, Sandra Oswald alitoa vocha mbili zenye thamani ya sh laki 5 kila moja kwa Fatma Omar Kibwana na Fadhila Athumani Mgumia walioibuka washindi katika mashindano ya TELS biashara kiosk ambapo wataitumia kama mitaji ya katika biashara zao.

Leave a Comment