×

Marekani Yafanya Mashambulizi Mapya Iran Baada ya Meli Tatu Kushambuliwa Hormuz

Jeshi la Marekani limetekeleza mashambulizi mapya dhidi ya Iran mapema Jumatano, saa chache baada ya meli tatu za kibiashara kushambuliwa katika Mlango wa Hormuz, hatua inayoongeza mvutano na kuhatarisha makubaliano ya muda yaliyolenga kusitisha mapigano kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la “kuigharimisha Iran kutokana na kulenga na kushambulia meli za kibiashara zilizokuwa zikiendeshwa na raia wasio na hatia katika njia ya kimataifa ya majini.”

Marekani imeieleza hatua ya Iran kuwa ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na kitendo kinachohatarisha usalama wa usafiri wa kimataifa katika Mlango wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani.

Taarifa zinaeleza kuwa moja ya meli hizo ilipigwa na kombora karibu na pwani ya Oman na kushika moto, huku meli nyingine mbili zikipata uharibifu mdogo lakini kuendelea na safari zao. Hakuna taarifa za majeruhi zilizoripotiwa.

Wakati huo huo, Marekani imefuta leseni iliyokuwa ikiruhusu mauzo ya mafuta ya Iran, ikisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mashambulizi yaliyofanyika dhidi ya meli katika Mlango wa Hormuz.

Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekosoa uamuzi huo wa Marekani, ikidai kuwa unakiuka makubaliano ya muda yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, pia ameeleza kuwa mashambulizi mapya ya Marekani yanakiuka makubaliano hayo.

Nayo Qatar imelaani shambulio dhidi ya moja ya meli zake za gesi asilia, ikilitaja kuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na usalama wa usafiri wa baharini, huku ikiishutumu Iran kubeba jukumu la kisheria kwa tukio hilo.

Wakati huohuo, mazungumzo kati ya Marekani na Iran yanaelezwa kusimama kwa muda, huku Iran ikiendelea na maandalizi ya mazishi ya Kiongozi wake Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei, ambaye kwa mujibu wa taarifa hizo aliuawa mwanzoni mwa vita.

Endapo hali itaendelea kuwa tete katika Mlango wa Hormuz, wachambuzi wanaonya kuwa usafirishaji wa mafuta na gesi duniani unaweza kuathirika, jambo litakaloongeza shinikizo kwa uchumi wa kimataifa.

Leave a Comment