
ANKARA, Uturuki: Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran “yamefikia mwisho” baada ya Iran kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani katika Mashariki ya Kati usiku wa kuamkia Jumatano.
Akizungumza mjini Ankara, Uturuki, Trump aliishutumu Iran kwa kuvunja makubaliano hayo na kuielezea serikali ya Tehran kuwa imefanya mchezo mchafu kwa kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Kuwait.
“Kwa mtazamo wangu, makubaliano hayo yamekwisha. Nimeongea na wawakilishi wetu, wanataka kuendelea na mazungumzo, lakini kwangu mimi ni kupoteza muda kushughulika nao,” alisema Trump.
Rais huyo aliendelea kuikosoa Iran, akiitaja kuwa ni serikali yenye viongozi wenye msimamo mkali na kudai kuwa iwapo wangekuwa na silaha za nyuklia wangezitumia.

Kauli hiyo imekuja baada ya Marekani kutekeleza mashambulizi makubwa ya kulipiza kisasi dhidi ya zaidi ya malengo 80 ya kijeshi nchini Iran kufuatia mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Mlango wa Hormuz.
Katika taarifa yake, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema mashambulizi hayo yalilenga mifumo ya ulinzi wa anga, maeneo ya kurushia makombora ya ardhini kwenda angani, vituo vya kurushia droni, miundombinu ya bandari, mifumo ya ufuatiliaji wa pwani pamoja na maeneo ya makombora ya kupambana na meli.
CENTCOM ilisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Iran kushambulia meli za kibiashara zilizokuwa zikisafiri katika njia za kimataifa za baharini, jambo ambalo ilidai ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Milipuko iliripotiwa katika miji ya bandari ya Bandar Abbas, Sirik na katika Kisiwa cha Qeshm, maeneo ambayo yamekuwa yakilengwa na mashambulizi ya Marekani katika miezi ya hivi karibuni.
Wakati huo huo, televisheni ya taifa ya Iran ilidai kuwa meli moja ilishambuliwa baada ya kupuuza maonyo, lakini haikusema ni nani aliyekuwa nyuma ya tukio hilo.
Mvutano huo umejiri wakati Mlango wa Hormuz ukiendelea kuwa kitovu cha mgogoro kati ya Iran, Marekani na Israel tangu mwishoni mwa Februari, kutokana na umuhimu wake katika usafirishaji wa mafuta duniani.
Mnamo Juni 17, Trump na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian walikuwa wamefikia makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano na kuanzisha mazungumzo ya amani. Sehemu ya makubaliano hayo iliruhusu meli kupita katika Mlango wa Hormuz bila kutozwa ada kwa siku 60, huku Iran ikisisitiza kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia njia hiyo.

Hata hivyo, mashambulizi ya hivi karibuni yamezua hofu kuwa mazungumzo hayo yanaweza kuvunjika kabisa.
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, alijibu kupitia mtandao wa X akisema: “Enzi za vitisho na uonevu zimekwisha. Hatuwezi kusalimu amri.”
Trump pia alidai kuwa Iran inaonyesha nia ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo, huku akionya kuwa Marekani iko tayari kuchukua hatua kali zaidi ikiwa mashambulizi yataendelea.
Kauli hizo zimetolewa wakati Trump akihudhuria mkutano wa viongozi wa NATO mjini Ankara, ambapo pia amezikosoa baadhi ya nchi wanachama wa muungano huo kwa kusuasua kutoa ushirikiano wa kijeshi katika operesheni dhidi ya Iran.
