×

Mwanamapinduzi wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa Al-Thani Afariki

DOHA: Aliyekuwa Emir wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Al-Thani, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74, baada ya kuiongoza nchi hiyo kupitia kipindi kilichoshuhudia mageuzi makubwa yaliyoiweka Qatar miongoni mwa mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani.

Taarifa ya kifo chake ilitangazwa Jumapili na Ofisi ya Emir wa Qatar (Amiri Diwan), hata hivyo haikueleza chanzo cha kifo hicho.

Sheikh Hamad aliingia madarakani mwaka 1995 baada ya kumng’oa madarakani baba yake, Sheikh Khalifa bin Hamad Al-Thani, katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu akiwa baba yake yuko nje ya nchi.

Katika kipindi chake cha uongozi, alisimamia mageuzi makubwa yaliyoibadilisha Qatar kutoka taifa dogo la jangwani na kuwa moja ya nchi tajiri zaidi duniani kupitia sekta ya mafuta na gesi asilia. Pia alipanua ushawishi wa Qatar katika diplomasia, uchumi na uwekezaji wa kimataifa.

Mwaka 2013, Sheikh Hamad aliweka historia kwa kuachia madaraka kwa hiari na kumkabidhi mwanawe, Emir wa sasa, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani. Katika hotuba yake ya kujiuzulu, alisema ulikuwa wakati wa kizazi kipya kuchukua nafasi ya uongozi kwa mawazo mapya na nguvu mpya.

Hatua hiyo ilivunja utamaduni uliokuwa umezoeleka katika tawala za kifalme za Ghuba, ambapo viongozi wengi hubaki madarakani hadi mwisho wa maisha yao.

Urithi wa Sheikh Hamad unaonekana katika maendeleo makubwa ya Qatar, ikiwemo ukuaji wa uchumi, kuimarika kwa nafasi yake katika siasa za kimataifa na kujijengea hadhi kama moja ya mataifa yenye ushawishi mkubwa katika Mashariki ya Kati.

Kifo chake kimeacha majonzi nchini Qatar na katika jumuiya ya kimataifa, huku akitambulika kama mmoja wa viongozi waliobadili kwa kiasi kikubwa historia ya taifa hilo.

Leave a Comment