×

Fahamu Kesi ya Mauaji ya Msichana Celeste wa Miaka 14 Iliyotikisa Marekani, D4vd Akamatwa

Celeste Rivas Hernandez, msichana mwenye umri wa miaka 14 kutoka California, Marekani enzi za uhai wake.

Kesi ya mauaji ya Celeste Rivas Hernandez, msichana mwenye umri wa miaka 14 kutoka California, Marekani, imeendelea kuvuta hisia za watu wengi baada ya waendesha mashtaka kutoa maelezo mapya yanayomkabili mwanamuziki David Anthony Burke, anayejulikana kwa jina la kisanii D4vd.

Celeste alitangazwa kupotea mwaka 2024 baada ya kutoweka bila kujulikana aliko. Polisi walisema aliwahi kutoroka nyumbani, akarudi, kisha kutoweka tena, hali iliyoifanya familia yake na mamlaka kuanzisha msako mkubwa wa kumtafuta.

Miezi kadhaa baadaye, Septemba 2025, uchunguzi ulichukua mwelekeo mpya baada ya mabaki ya mwili wake kupatikana ndani ya sehemu ya mbele ya gari aina ya Tesla (frunk) lililosajiliwa kwa jina la Burke na kutelekezwa katika eneo la Hollywood Hills, Los Angeles.

Ripoti ya daktari bingwa wa uchunguzi wa maiti ilibaini kuwa Celeste alifariki kutokana na majeraha yaliyosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali, huku kifo chake kikitangazwa rasmi kuwa ni mauaji. Uchunguzi pia ulieleza kuwa mwili ulikuwa umeharibika kiasi cha kuchelewesha kubaini chanzo halisi cha kifo.

Baada ya miezi kadhaa ya uchunguzi, Burke alikamatwa mwezi Aprili 2026 na kufunguliwa mashtaka mbalimbali, ikiwemo mauaji, madai ya kufanya vitendo vya kingono dhidi ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 14, pamoja na shtaka la kuharibu au kuficha ushahidi kwa kuudhalilisha mwili wa marehemu.

Sasa, waendesha mashtaka wamewasilisha nyaraka mpya mahakamani zikieleza kwa kina mazingira wanayodai yalipelekea mauaji hayo.

Mwanamuziki David Anthony Burke, anayejulikana kwa jina la kisanii D4vd.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Burke anadaiwa kuanza kumfahamu Celeste alipokuwa na umri wa miaka 11, huku uhusiano wa kimapenzi na kingono ukidaiwa kuanza msichana huyo alipofikisha miaka 13, wakati Burke akiwa na miaka 18.

Waendesha mashtaka wanadai Celeste alitishia kuweka hadharani taarifa ambazo zingeharibu maisha binafsi na taaluma ya muziki ya Burke. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, hofu hiyo ndiyo iliyomfanya msanii huyo kupanga kumuua.

Nyaraka hizo zinadai kuwa muda mfupi baada ya Celeste kufika nyumbani kwa Burke, alidaiwa kumchoma kisu mara kadhaa na kumwacha akivuja damu hadi kufariki dunia.

Aidha, waendesha mashtaka wanadai siku iliyofuata Burke alinunua misumeno miwili ya umeme (chainsaws) na kuitumia kuukatakata mwili wa marehemu ndani ya bwawa la plastiki (inflatable pool), huku DNA ya Celeste ikidaiwa kupatikana kwenye gereji ya nyumba ya msanii huyo.

Mbali na hilo, upande wa mashtaka unadai Burke alikuwa akihifadhi picha za unyanyasaji wa kingono zinazomhusisha Celeste.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani pia unajumuisha rekodi za mawasiliano ya simu zinazodaiwa kuonyesha Celeste alikuwa akionesha wivu kutokana na mahusiano ya Burke na wanawake wengine, huku akiamini walikuwa na mpango wa kuwa pamoja siku zijazo. Waendesha mashtaka wanadai pia msichana huyo alitishia kufichua taarifa kuhusu uhusiano wao ambazo zingeharibu kazi ya msanii huyo.

Katika madai mengine, waendesha mashtaka wanasema baada ya wazazi wa Celeste kumchukua simu yake, Burke alimlipa rafiki wa msichana huyo dola za Marekani 1,000 ili ampatie simu nyingine waweze kuendelea kuwasiliana. Pia wanadai Celeste aliishi kwa muda katika nyumba ya Burke huko Hollywood Hills na kusafiri naye kwenda Las Vegas, London na Texas, ambako alikutana na familia ya msanii huyo.

Hata hivyo, mawakili wa Burke wamekanusha tuhuma zote zinazomkabili mteja wao, wakisisitiza kuwa hana hatia na hakuhusika na mauaji ya Celeste. Pia waliomba mahakama izuie nyaraka za upande wa mashtaka kutolewa kwa umma, lakini ombi hilo lilikataliwa.

Kesi hiyo inaendelea katika mahakama ya California, huku usikilizwaji wake ukitarajiwa kuendelea baada ya kuahirishwa ili kuwapa mawakili wa utetezi muda wa kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.

Kwa sasa, madai yote yaliyotolewa na waendesha mashtaka bado hayajathibitishwa mahakamani. Burke ameomba kutokuwa na hatia, na kwa mujibu wa sheria za Marekani, anaendelea kuchukuliwa kuwa hana hatia hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho.

Leave a Comment