×

Kombe la Dunia 2026 Kusafirishwa kwa Sanduku Maalum la Louis Vuitton

NEW YORK: Kombe la Dunia la FIFA litasafirishwa kuelekea Uwanja wa New York-New Jersey kwa kutumia sanduku maalum la kifahari lililotengenezwa na kampuni maarufu ya mitindo ya Ufaransa, Louis Vuitton.

Sanduku hilo maalum limebuniwa kwa ajili ya kubeba kombe lenye thamani kubwa zaidi katika soka duniani, likiwa na alama ya dhahabu yenye herufi “V” inayowakilisha neno Victory (ushindi) pamoja na jina la chapa hiyo, Vuitton.

Muundo wa sanduku hilo umejumuisha michoro maarufu ya Louis Vuitton, pembe zilizopakwa shaba ya dhahabu na ndani yake limewekewa ngozi laini ya rangi ya beige pamoja na alama maalum ya kuadhimisha ushirikiano kati ya Louis Vuitton na FIFA.

Hii ni mara ya tano mfululizo kwa kampuni hiyo ya kifahari kubuni sanduku la kubebea Kombe la Dunia, baada ya kufanya hivyo katika michuano ya mwaka 2010, 2014, 2018 na 2022.

Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Louis Vuitton, Pietro Beccari, amesema ushirikiano wao na FIFA umejengwa kwa zaidi ya muongo mmoja kwa lengo la kuonyesha ubora na nguvu ya michezo katika kuunganisha watu duniani.

“Kwa zaidi ya muongo mmoja, Louis Vuitton na FIFA wameshiriki dhamira ya pamoja ya ubora, wakiamini nguvu ya michezo kuhamasisha na kuwaunganisha watu,” alisema Beccari.

Makampuni ya kifahari yamekuwa yakishirikiana kwa karibu na michezo mikubwa duniani, ambapo Tiffany & Co. hutengeneza kombe la mabingwa wa Super Bowl nchini Marekani, linalojulikana kama Vince Lombardi Trophy, tangu mwaka 1967.

Louis Vuitton pia hutengeneza masanduku maalum ya kubebea mataji ya mashindano makubwa ya magari ya Formula 1 kupitia makubaliano ya miaka 10.

Hata hivyo, tofauti na mataji mengine, Kombe la Dunia la FIFA lina nafasi ya kipekee kwa kuwa ni kombe moja pekee linalotolewa kila baada ya miaka minne na kwa kawaida huhifadhiwa katika Makumbusho ya FIFA jijini Zurich, Uswisi.

Leave a Comment