
Mwanamuziki maarufu wa Colombia, Shakira, amempa sifa kubwa nahodha wa Argentina, Lionel Messi, pamoja na mke wake Antonela Roccuzzo, kabla ya mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Hispania.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Shakira alieleza kuvutiwa na kiwango cha Messi katika michuano hiyo, akisema mafanikio ya nyota huyo yanaonyesha nidhamu, kujituma na uwezo wa kupambana dhidi ya changamoto.
“Anachofanya Lionel Messi ni zaidi ya kuwa cha kawaida. Kinaonyesha maadili ya mtu mwenye kujitolea na nidhamu kubwa,” aliandika Shakira.

Messi, mwenye umri wa miaka 39, amekuwa miongoni mwa wachezaji bora kwenye michuano hiyo, akiwa amefunga jumla ya mabao nane sawa na mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappé, huku akiiongoza Argentina kufika fainali baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya England kwenye hatua ya nusu fainali.
Shakira pia alimpongeza Antonela Roccuzzo kwa nafasi yake katika maisha ya Messi, akisema kuwa kuwa na mwanamke kama Antonela pembeni yake kunampa nguvu na hamasa zaidi ya kuendelea kufanya vizuri.
“Najua kuwa kuwa na mwanamke kama Antonela pembeni yake kunampa nguvu na msukumo wa kuthibitisha uwezo wake,” alisema Shakira.

Antonela naye alijibu ujumbe huo kwa kuushiriki tena kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa ameambatanisha na emoji ya machozi na moyo mweupe.
Wakati huo huo, Shakira ataingia kwenye historia ya Kombe la Dunia baada ya kutangazwa kuwa mmoja wa wasanii watakaotumbuiza kwenye mapumziko ya fainali (halftime show) kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo, sambamba na mastaa wengine kama Madonna, BTS na Justin Bieber.
Fainali ya Kombe la Dunia 2026 kati ya Argentina na Hispania inatarajiwa kupigwa Jumapili, Julai 19, katika Uwanja wa New York-New Jersey.