
Klabu ya Inter Miami imetangaza rasmi kumsajili kiungo mkongwe wa Brazil, Casemiro, kama mchezaji huru baada ya kuondoka Manchester United mwishoni mwa msimu uliopita.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 amesaini mkataba wa kuitumikia Inter Miami hadi mwisho wa msimu wa MLS wa mwaka 2027, ukiwa na kipengele cha kuongeza hadi Juni 2029.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kutangazwa kwa usajili huo, Ligi Kuu ya Marekani (MLS) ilitangaza kuanzisha uchunguzi kuhusu madai ya ukiukwaji wa kanuni za usajili (tampering), hatua iliyotia doa ujio wa Casemiro nchini humo.
MLS imesema Inter Miami na LA Galaxy walifikia makubaliano kuhusu haki za usajili (Discovery Priority Rights) za Casemiro, lakini masharti ya makubaliano hayo hayatatangazwa hadi uchunguzi utakapokamilika.
Kwa mujibu wa kanuni za MLS, klabu inayotaka kumsajili mchezaji kutoka nje ya mfumo wa draft au usajili wa wachezaji huru lazima kwanza ijadiliane na klabu inayoshikilia haki za awali za mchezaji huyo. Kabla ya Casemiro kujiunga Inter Miami, haki hizo zilikuwa zinashikiliwa na LA Galaxy.
Ligi hiyo haijaeleza adhabu zinazoweza kutolewa wala muda ambao uchunguzi huo utakamilika.
Casemiro anaingia Inter Miami akiwa na rekodi kubwa ya mafanikio. Akiwa Real Madrid alitwaa mataji matano ya UEFA Champions League na mataji matatu ya La Liga kabla ya kuhamia Manchester United mwaka 2022, ambako alisaidia timu hiyo kutwaa Kombe la Carabao na FA Cup.
Katika ngazi ya kimataifa, Casemiro ameichezea Brazil mara 91, akishinda Copa America 2019 na kushiriki Kombe la Dunia mara tatu. Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil kilichoishia hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kutolewa na Norway.