×

Makosa 7 Yaliyosababisha Ajali ya Meli ya Costa Concordia na Vifo vya Watu 32

Ajali ya meli ya kifahari Costa Concordia iliyotokea Januari 13, 2012, na kusababisha vifo vya watu 32 imeendelea kukumbukwa kama moja ya majanga makubwa zaidi katika historia ya usafiri wa baharini. Sasa simulizi hilo limeangaziwa upya kupitia filamu ya Netflix Shipwrecked: Nightmare at Sea.

Meli hiyo ilikuwa imeondoka bandarini karibu na Roma, Italia, ikiwa na abiria 3,206 na wafanyakazi 1,023 kwa safari ya siku saba katika Bahari ya Mediterania.

Hata hivyo, safari hiyo iligeuka kuwa janga baada ya Nahodha Francesco Schettino kubadili njia iliyopangwa ili kupita karibu na Kisiwa cha Giglio kama ishara ya salamu.

Miongoni mwa makosa makubwa yaliyobainika ni kushindwa kupunguza mwendo wa meli ilipokaribia ufukweni, hali iliyosababisha igonge mwamba uliokuwa chini ya maji na kupasuka sehemu ya ubavu wake. Maji yaliingia haraka kwenye chumba cha injini, na meli ikapoteza umeme pamoja na uwezo wa kuongozwa.

Nahodha Francesco Schettino

Ripoti pia zinaeleza kuwa kulikuwa na changamoto ya mawasiliano kati ya nahodha na rubani wa usukani kutokana na tofauti za lugha, jambo ambalo huenda lilichangia kuchelewa kubadili mwelekeo wa meli.

Aidha, Schettino alidai kifaa muhimu cha kurekodi taarifa za urambazaji kilikuwa hakifanyi kazi ipasavyo, huku ikielezwa pia kuwa alikuwa akiiongoza meli kwa kutegemea uzoefu wake binafsi na macho badala ya kutumia kikamilifu rada na mfumo wa kisasa wa urambazaji.

Meli ya ‘Costa Concordia’ Januari 2012 kama ilivyoonekana katika filamu ya Shipwrecked: Nightmare at Sea.

Baada ya ajali kutokea, nahodha aliwaambia abiria kuwa kulikuwa na hitilafu ya umeme pekee na akachelewesha kutoa tahadhari rasmi ya dharura. Pia aliliambia Jeshi la Walinzi wa Pwani la Italia kuwa hali ilikuwa inadhibitiwa, licha ya kujua kuwa maji yalikuwa yakiendelea kujaa ndani ya meli.

Amri ya kuwaamuru abiria kuondoka melini ilitolewa zaidi ya saa moja baada ya ajali, jambo lililosababisha vurugu kubwa wakati wa uokoaji. Kufikia wakati huo, baadhi ya boti za uokozi zilishindwa kuteremshwa kutokana na meli kuelemea upande mmoja.

Baada ya uchunguzi, Nahodha Schettino alipatikana na hatia ya kusababisha ajali, kuua kwa uzembe na kuitelekeza meli kabla ya kuhakikisha abiria wote wameokolewa.

Alihukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 16 gerezani, huku maafisa wengine wa kampuni ya meli hiyo wakikabiliwa na mashtaka ya uzembe na baadaye kukubaliana na makubaliano ya kisheria.

Ajali hiyo ilisababisha mabadiliko katika sheria za usalama wa usafiri wa baharini, ikiwemo kuweka masharti mapya kuhusu upatikanaji wa makoti ya kuokoa maisha na taratibu za uokoaji kwa meli za watalii.

Makosa 7 yaliyotajwa kuchangia ajali ya Costa Concordia:

  1. Kubadili njia ya safari bila sababu ya kiusalama – Nahodha Francesco Schettino aliondoa meli kwenye njia rasmi ili kupita karibu na Kisiwa cha Giglio kwa ajili ya kutoa salamu, hatua iliyoiweka meli katika eneo hatari.
  2. Kutopunguza mwendo wa meli – Licha ya kukaribia ufukweni, meli iliendelea kwenda kwa kasi ya takribani mafundo 16 (karibu kilomita 30 kwa saa) hadi ilipogonga mwamba uliokuwa chini ya maji.
  3. Hitilafu za mawasiliano darajani – Uchunguzi ulionyesha kuwa kulikuwa na changamoto za lugha kati ya nahodha na rubani wa usukani, jambo lililochangia kuchelewa kutekeleza maagizo ya kubadili mwelekeo.
  4. Kutotumia kikamilifu rada – Nahodha aliamua kuiongoza meli kwa kutegemea macho na uzoefu wake wa awali badala ya kutegemea vifaa vya kisasa.
  5. Kuchelewesha kutangaza hali ya dharura – Badala ya kuwatahadharisha abiria mara moja, nahodha aliwaeleza kuwa meli ilikuwa imepata hitilafu ya umeme, jambo lililosababisha watu wengi kubaki bila kuelewa ukubwa wa hatari.
  6. Kuchelewa kutoa amri ya kuondoka melini – Amri ya kuanza uokoaji ilitolewa zaidi ya saa moja baada ya meli kugonga mwamba, wakati maji tayari yalikuwa yamejaa ndani ya sehemu za chini za meli.
  7. Changamoto katika uokoaji – Meli ilipoanza kuelemea upande mmoja, baadhi ya boti za uokozi zilishindwa kuteremshwa. Pia, baadhi ya abiria walishindwa kufikia makoti ya kuokoa maisha kwa urahisi kutokana na meli kuegemea, hali iliyoongeza taharuki na kuathiri operesheni ya uokoaji.

Makosa hayo yalitajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu zilizosababisha ajali hiyo mbaya iliyogharimu maisha ya watu 32 na kujeruhi mamia ya wengine, huku ikisababisha mageuzi makubwa katika kanuni za usalama wa meli za watalii duniani.

Leave a Comment