
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ahadi ya kupatikana kwa Katiba Mpya nchini bado ipo na itaendelea kutekelezwa, kwani ni ahadi iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ambaye pia amepongeza kauli ya Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi ya kusisitiza dhamira ya Serikali na CCM kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana.
Mbeto amesema ahadi hiyo ilitolewa na Rais Samia wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa CCM katika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam, na kwamba kauli ya Dkt. Nchimbi inaendana moja kwa moja na maamuzi ya chama na Serikali.
“Napenda kumpongeza Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi kwa kuwakumbusha Watanzania kuhusu ahadi ya Katiba Mpya. CCM ndiyo iliyoruhusu mfumo wa vyama vingi na ndiyo itakayohakikisha Katiba Mpya inapatikana,” alisema Mbeto.
Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kukiamini CCM, akieleza kuwa maamuzi makubwa yanayohusu maslahi ya taifa hufanyika kwa umakini, baada ya tathmini na uchambuzi wa kina, badala ya kufanywa kwa haraka au chini ya shinikizo.
Mbeto aliongeza kuwa kauli zinazotolewa na Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu hutokana na maamuzi ya pamoja ya chama na Serikali kupitia vikao rasmi vya maamuzi.
Pia alisema Katiba ya mwaka 1977 imeendelea kuliongoza taifa kwa zaidi ya miongo sita, lakini iwapo Watanzania wataamua kupata Katiba Mpya, mchakato huo unapaswa kufanyika kwa njia za mazungumzo ya amani na ushirikishwaji, bila vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.
Kwa mujibu wa Mbeto, jukumu la kuandaa Katiba Mpya ni la Watanzania wenyewe, huku Serikali ya CCM ikiwa na wajibu wa kuweka mazingira wezeshi yatakayowezesha kupatikana kwa katiba itakayokidhi mahitaji ya wakati na matakwa ya wananchi.