×

Filamu ya “The Odyssey” Yafikisha Bilioni 801 Kwa Siku 12, Yavutia Watazamaji

Filamu ya “The Odyssey” imeendelea kufanya vizuri katika mauzo ya tiketi duniani, ikifikisha mapato ya takribani dola milioni 304 sawa TSh bilioni 801.3 ndani ya siku 12 tangu kuanza kuonyeshwa, huku ikiendelea kuvutia watazamaji wengi.

Mafanikio hayo yamekuja licha ya ukosoaji kutoka kwa Emily Wilson, mtaalamu wa tafsiri ya kazi ya kale ya Homer, The Odyssey, ambaye amekosoa kwa ukali filamu hiyo inayoongozwa na mtengenezaji filamu Christopher Nolan.

Wilson, ambaye alifanya tafsiri maarufu ya kitabu hicho kwenda Kiingereza, alieleza kutoridhishwa kwake na baadhi ya vipengele vya filamu hiyo, akisema asingependa kuhusishwa na uandishi wa sehemu ya maandishi ya filamu hiyo.

Hata hivyo, mafanikio ya kibiashara ya filamu hiyo yanaendelea kuonyesha kuwa ukosoaji huo haujazuia watazamaji kuendelea kwenda kuitazama.

Kutokana na umaarufu wa filamu hiyo, jina la Homer na simulizi la kale la The Odyssey limeendelea kupata umaarufu zaidi, huku baadhi ya matoleo ya kitabu hicho yakiongezeka katika mauzo kwenye maduka ya vitabu mtandaoni.

Filamu hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya sinema ya mwaka huu, huku ikitarajiwa kuvuka zaidi ya dola milioni 400 sawa TSh trilioni 1.05 ikiwa itaendelea kupata mwitikio huo wa watazamaji.

Mbali na The Odyssey, filamu nyingine iliyopata mafanikio hivi karibuni ni toleo la sinema la muziki wa Broadway “Hadestown”, ambalo limeanza kufanya vizuri katika siku zake za mwanzo baada ya kuingizwa kwenye mfumo wa filamu.

Mafanikio ya miradi hiyo yanaendelea kuongeza mjadala kuhusu namna kazi za jukwaani na fasihi za zamani zinavyoweza kufikishwa kwa hadhira kubwa kupitia sinema.

Leave a Comment