×

Dkt. Mwigulu: Uwekezaji wa Utafiti wa Kilimo ni Msingi wa Mageuzi ya Sekta

Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, amesema kuwa kuwekeza katika utafiti wa kilimo ndiyo njia sahihi ya kuleta mageuzi ya kweli katika sekta hiyo na kuongeza tija kwa wakulima nchini.

Akizungumza leo Agosti 2, 2026, Iyumbu jijini Dodoma wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa makao makuu ya Agricultural Inputs Trust Fund (AGITF), Dkt. Mwigulu alisema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya taasisi zinazohudumia wakulima ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Alisisitiza kuwa uwekezaji wa majengo na miundombinu unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Tunachokijenga hapa si jengo pekee, bali ni mazingira bora ya utendaji wa mfuko. Watumishi wote wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa bidii ili uwekezaji huu uwe na manufaa kwa Taifa. Tusiwe na ofisi nzuri halafu huduma zikawa duni,” alisema.

Waziri Mkuu alisema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika taasisi za utafiti wa kilimo unaonesha dhamira ya dhati ya kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa na yenye tija.

Alibainisha kuwa maabara mpya ya kisasa ya kilimo pamoja na makao makuu ya Tanzania Agricultural Research Institute (TARI) ni vielelezo vya dhamira hiyo.

“Kwa nchi nyingine maabara ya kiwango hicho ingekuwa katika chuo kikuu, lakini kwetu ni maabara ya Wizara ya Kilimo. Hii inaonyesha jinsi Serikali ilivyojipanga kufanya mageuzi ya kilimo,” aliongeza.

Dkt. Mwigulu pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo jijini Dodoma na kwa kuwaamini wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mikubwa ya Serikali.

Alisema hatua hiyo imechangia kukuza uchumi wa ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uwezo wa kampuni za ndani kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuongeza bajeti ya wizara hiyo, jambo ambalo limeiwezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuimarisha sekta ya kilimo nchini.

Leave a Comment