×

Video: Hersi Awataka Wanachama wa Yanga Kuvunja Makundi Baada ya Uchaguzi, Watano Wachaguliwa

Wanachama wa Yanga wamewachagua wajumbe watano wapya wa Kamati ya Utendaji katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa SuperDome, Masaki jijini Dar es Salaam.

Waliochaguliwa kushika nafasi hizo ni Yanga Makaga, Alex Ngai, Julius Koyi, Munir Said na Fahd Afif, baada ya kuibuka washindi katika uchaguzi uliofanyika wakati wa mkutano huo.

Uchaguzi huo ni sehemu ya mchakato wa kuimarisha uongozi wa klabu, ambapo wajumbe hao wanatarajiwa kushiriki katika maamuzi na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya Yanga ndani na nje ya uwanja.

Akihutubia wanachama baada ya uchaguzi huo, Rais wa Yanga, Hersi Said, aliyefanikiwa kutetea nafasi yake, amewataka wanachama kuweka pembeni tofauti zilizojitokeza wakati wa kampeni na kuvunja makundi yaliyoundwa kipindi cha uchaguzi.

Hersi alisema uchaguzi umekamilika na sasa ni wakati wa wanachama wote kuungana kwa ajili ya maslahi ya klabu, akisisitiza kuwa wagombea ambao hawakufanikiwa hawapaswi kuyachukulia matokeo hayo kwa chuki kwani bado ni sehemu muhimu ya familia ya Yanga.

Amesema mshikamano na umoja vitakuwa msingi muhimu katika kuendeleza mafanikio ya klabu kuelekea msimu mpya wa mashindano.

Leave a Comment